Usikose Hizi Hapa

MAADHIMISHO YA SIKU YA KISUKARI DUNIANI YAANZA LEO DAR NA KAMPENI YA MAZOEZI

Asilimia 27 ya vifo vyote nchini na asilimia 60 ya vifo vyote Duniani vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo mwaka 2005 katika vifo milioni 58 vilivyotokea Duniani,vifo milioni 35 vilitokana na magonjwa hayo.

Tamko hilo limetolewa  na Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  Dkt Neema Rusibamayila ,wakati wa  wa matembezi ya maadhimisho ya Siku ya kisukari Duniani pamoja na Maadhimisho ya Kampeni ya Mazoezi yaliyoanza leo katikaViwanja vya mpira Muhimbili hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Dkt Neema amesema Utafiti wa Viashiria vya magonjwa yasiyo ya Kuambukiza uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) mwaka 2012 unaonyesha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo 15.9% ya wananchi wanavuta sigara,asilimia 29.3% wanakunywa pombe,asilimia 97.2% wanakula mbogamboga na matunda chini ya mara tano kwa wiki.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani inakadiriwa kuwa asilimia 20 ya vifo vyote vilivyotokea nchini mwaka 2005 vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo magonjwa ya moyo ni asilimia 9%,saratani ni asilimia 4,magonjwa ya mfumo wa hewa ni asilimia 2%,kisukari asilimia 1 na magonjwa mengine sugu ni asilimia 4%.

Aidha utafiti ulionyesha asilimia 26% ya wananchi ni wanene kupita kiasi,asilimia 26% wana lehemu nyingi mwilini,asilimia 33.8% wana mafuta mengi mwilini,asilimia 9.1% wana kisukari na asilimia 25.9% wana shinikizo kubwa la damu.

Pamoja na hayo utafiti pia ulionyesha asilimia 25% ya wananchi waliohojiwa hawajishugulishi na kazi zinazotumia nguvu na hawafanyi mazoezi ambapo asilimia 6% ya vifo Duniani huchangiwa na kutofanya mazoezi na ni kiashiria cha nne Duniani kinachochangia vifo ambapo inakadiriwa kuwa kutofanya mazoezi kuacgangia asilimia 17 ya magonjwa ya moyo na kisukari,asilimia 12 ya matatizo ya kuanguka na asilimia 10 ya saratani ya matiti na saratani ya utumbo mpana.

Aidha Dokta Neema ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao katika vituo vya afya na kuwahimiza kufanya mazoezi mara kwa mara,kuacha matumizi ya unywaji pombe kupita kiasi,matumizi ya tumbaku na bidhaa zake kama sigara,shisha na ugoro,ulaji usiofaa hasa matumizi ya chmvi kwa wingi,mafuta na sukari ili kuepukana na magonjwa hayo hatarishi hasa kwa nchi zilizoendelea.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Kisukari Duniani yaliyohudhuriwa na taasisi mbalimbali,mashirika binafsi na ya kiserikali ndani na nje ya nchi yenye kauli mbiu ya Wanawake na Kisukari;Haki ya Afya Bora ya baadae hufanyika Novemba 11 kila mwaka ambapo mwaka huu kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe 14 Novemba.






No comments