Darassa ana fursa ya kuingiza mamilioni ya shilingi kwa show za Kenya
Akiwa anajitayarisha kutoa album yake mwaka huu wa 2017, rapper Darassa hivi sasa ana uwezo wa kujiunga na wanamuziki wa kuimba wa Bongo Flava nguli Diamond Platnumz, Rais CEO wa kampuni ya muziki Africa WCB na hasimu wake wajadi kimuziki si mwingine bali ni Mfalme wa Bongo Flava Africa Alikiba, kwa kuwachuna Wakenya mamilioni ya pesa kwa hiyari yao kupitia ufanisi wake kimuziki na umaarufu unaozidi kupanda kila uchao hapa nchini Kenya.
Nikianzia na mjini Mombasa uswahilini hapa, nakupatia hali halisi jinsi ilivyo. Nakutembeza katika mitaa kadha wa kadha ambapo mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wameupokea wimbo wa rapper Darassa ‘Muziki’ kwa taadhima na heshima kubwa. Kuanzia kitongoji cha Lights, Soko Mjinga, Kisauni, Mwandoni, Mtopanga, Bombolulu, Bamburi hadi kuvuka ng’ambo ya pili ya Ferry Likoni mpaka Ukunda nyimbo, ‘Muziki’ inatamba kwa kasi zaidi ya mawimbi mazito baharini.
Mbali na Pwani ya Kenya, sehemu za nyanda za juu na Ziwa Victoria hadi Kisumu na Kenya yote kwa jumla. Kituo cha redio maarufu zaidi nchini cha Citizen, kupitia kipindi cha Mambo Mseto kinachoendeshwa na mtangazaji anayependwa sana na vijana Afrika Mashariki Mzazi Willy M Tuva, huwa kipimo kamili cha ni mwanamuziki gani anayetamba kwa sana Afrika Mashariki katika msimu fulani kwa kupitia requests zinazotumwa na mashabiki kwa kuitisha nyimbo za wasanii wanaowakubali.
Msimu huu Darassa ameivunja rekodi kwa jinsi nyimbo yake ya Muziki inavyoombwa kwa sana si radio Citizen pekee bali hadi vituo vingine mbalimbali hata vile vinavyotangaza kwa lugha ya jamii fulani ama lugha ya mama hapa Kenya.
Kimtazamo mji wa Mombasa ndio kitovu cha mafanikio kwa wasanii wengi wa Bongo Flava kutamba nchi Kenya wanaobobea na waliobobea na kufifia kimuziki. Nikiwataja baadhi tu wakiwemo Mr Nice ‘’Mzee wa Fagilia, Mr. Blue jamaa la ‘Mapozi’, Ray C ‘Mrembo wa Wanifuatia nini’, Lady Jaydee ‘Dada wa Siku hazigandi’, Proffessor Jay ‘Nguli wa Zali la Mentali’, Ferooz ‘Kigogo wa Starehe.’ Alikiba, ‘Jamaa wa Cinderella’, Diamond Platnumz ‘Raisi wa Kamwambie’ Yamoto Band ‘Vijana wa Nitakupelepweta’ na wengine wengi.
Hii inapelekewa na sababu ya kuwa watu wanaoishi katika pwani ya Kenya wengi wao hutumia Kiswahili na tokea jadi kabla ya muziki wa kizazi kipya kuiteka nyara anga ya muziki wa pwani nchini Kenya wamekuwa wakipenda sana muziki wa Taarabu ambao asili na chimbuko lake ni nchi ya Tanzania hivyo wa pwani wanajua utamu wa Bongo Flava kabla kusambaa sehemu zengine za nchi ya Kenya.
No comments