Usikose Hizi Hapa

KOREA KASKAZINI YASEMA MAZUNGUMZO NA MAREKANI HAYATOREJEA KARIBUNI

Korea Kaskazini imesema leo mazungumzo kuhusu mradi wake wa nyuklia na Marekani hayotaanza tena hadi utawala wa Rais Donald Trump utakapoachana na kile ilichokiita matwaka ya upande mmoja kwenye juhudi za kuuvunja mfumo wa nyuklia wa taifa hilo.
 
Shirika la habari la Korea Kaskazini limenukuu maoni ya msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo ambaye jina lake halikutajwa akiituhumu Marekani kwa kusababisha kwa makusudi kuvunjika mazungumzo ya mwezi Februari kati ya Rais Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. 

Afisa huyo amesema mazungumzo hayo yaliyofanyika nchini Vietnam yalivunjika kwa sababu ya matakwa ya upande mmoja yasiyotekelezeka. 

Maafisa wa Marekani wamesema mara kadhaa kuwa mkutano wa Trump na Kim ulivunjika kwa sababu Korea Kaskazini ilitaka kupewa nafuu ya vikwazo vilivyopo lakini kwa kuchukua hatua ndogo kuelekea kuachana na mradi wake wa nyuklia. 

Kim amesema Marekani ina hadi mwisho wa mwaka huu kuja na matakwa yanayokubaliwa na pande zote ili kuyanusuru mazungumzo hayo.

No comments