Zitto Kabwe Asakwa na Jeshi la Polisi kwa Uchochezi.....ACT Wazalendo Wadai Yuko Salama, Wataka Polisi Wafuate Utaratibu
Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo ndugu Msafiri A Mtemelwa ametoa taarifa kuwa kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Mh Zitto Kabwe hajakamatwa na polisi na kusema yupo salama hapa hapa nchini.
Akitumia mtandao wa twitter wa Chama cha ACT Wazalendo Msafiri Mtemelwa anadai kuwa kiongozi huyo wa chama yupo salama lakini dereva wake ndg Patrick Muhidin pamoja na katibu wa Chama wa jimbo la Kahama ndg. Vincent Ikerenge ndio walikamatwa na walipelekwa kituo cha polisi Kahama na kuandikishwa maelezo.
"Tunawajulisha kuwa kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe, Mb hajakamatwa na polisi na yupo salama hapa hapa nchini. Tarehe 21/1/2017 Polisi wilayani Kahama wakiwa na magari 7 kati yao manne ya FFU walivamia mkutano wa Kampeni wa Chama katika kata ya Isagehe, Halmashauri ya Mji wa Kahama. Kiongozi wa Chama alikuwa jukwaani wakati polisi wanafika na aliendelea na hotuba yake mpaka mwisho na kumnadi Mgombea ndg Ibrahim Masele. Baada ya kushuka jukwaani, Kama kawaida yake alipeana mikono na wananchi na baadaye alipotea katika eneo Hilo" alisema Msafiri Mtemelwa
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo ndugu Msafiri Mtemelwa anadai wamefuatilia polisi kutaka kujua kwanini kiongozi wa Chama chao anatafutwa na polisi na kusema wamejulishwa kuwa ana mashatka ya kutoa lugha ya uchochezi katika hotuba zake za kampeni.
"Tumejulishwa na polisi kwamba Kiongozi wa Chama ana mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi katika hotuba zake za kampeni katika kata ya Isagehe Jimbo la Kahama Mjini. Polisi wanasema Zitto Kabwe amemchonganisha Rais na wananchi kwa kusema kuwa Rais anakula bure na kulala bure ndio maana hajali hali ngumu ya maisha ya wananchi wakati huu wa balaa la njaa" ameandika Mtemelwa
Hata hivyo mbunge huyo wa Kigoma mjini na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kupitia viongozi wa chama cha ACT Wazalendo amesema polisi wataweza kumkamata iwapo yeye atataka kukamatwa na siyo kwa kuvamiwa bali kwa kuitwa rasmi na polisi na kuelezwa makosa yake.
"Chama kinalitaka jeshi la polisi kufuata taratibu za kukamata raia kwa mujibu wa sheria na pia protokali za kuwaita polisi viongozi wa Kitaifa Kama ilivyo kwa ndg Zitto. Chama kinajiandaa na wanasheria wake ili kwenda na KC kituo chochote cha polisi nchini Mara watakapopata wito wa kwenda polisi.". Amesema Msafiri Mtemelwa
CHANZO;MPEKUZI
No comments