Taarifa Ya Serikali Kutoka Bungeni Leo 02/02/2017
Dodoma, Alhamisi, 2 Februari, 2017: Serikali imetoa ufafanzi kuhusu masuala mbalimbali kuhusu utawala wa Sheria na kuainisha mikakati yake katika kuzuia au kupunguza athari za matetemeko ya ardhi nchini. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo.
Serikali Kutoingilia Mihimili ya Dola
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu mgawanyo wa mihimili mitatu ya dola nchini. Waziri Mkuu alikuwa akifafanua kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kesi zao zinachukua muda mrefu.
Aidha, Waziri Mkuu amekanusha vikali madai kuwa Serikali inakusudia au imetangaza kufuta vyama vya siasa hasa vya upinzani nchini madai yaliyotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe.
Mkakati Kuzuia Majanga Ya Asili
Akijibu hoja kuhusu mikakati ya kupambana na athari za majanga ya asili, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde, amesema Serikali tayari inao mkakati wa kitaifa wa kupambana na majanga ya asili yakiwemo matetemeko.
Aidha, Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo imeainisha aina mbalimbali za maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na majukumu ya kila mdau katika kushughulikia maafa. Aliongeza kuwa, Serikali pia imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Kukabiliana na Maafa ambao unaelekeza Taasisi kiongozi na wajibu wao wakati wa kukabiliana na majanga.
Liganga, Mchuchuma Kuzalisha Megawati 350
Serikali imesema kuwa, miradi unganishi ya Mchuchuma na Liganga itakayotekelezwa kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Group (SHG) Limited ya China kupitia ubia wa pamoja wa Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL) itazalisha zaidi ya ajira 33,000 na kuipatia nchi umeme wa megawati 350.
Akitoa ufafanuzi huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa kampuni hiyo imeshapewa leseni na vibali vingine muhimu na sasa inakamilisha ulipaji wa fidia ili kuanza kazi. “Miradi hiyo unganishi itawezesha kuchimbwa makaa ya mawe kiasi cha tani milioni (3) na chuma ghafi tani milioni 2.9 kwa mwaka,” alisema.
Usalama wa Raia Mipakani
Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo ya mipaka inachukua hatua za pamoja na vyombo vya nchi jirani kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao katika maeneo hayo.
Akijibu hoja kuhusu suala la usalama wa raia wanaoishi pembezoni mwa mipaka ya Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amefafanua kuwa operesheni za pamoja zinafanyika katika mipaka ya nchi na vikao vya ujirani mwema ili kuhakikisha usalama. Wananchi wameombwa kutoa taarifa wanapowaona wageni wasioeleweka katika maeneo yao ili kuimarisha usalama.
Wanahabari Waendeleze Kiswahili
Serikali imewapa changamoto wanahabari nchini kuwa chachu ya kuendeleza lugha ya Kiswahili. Wakijibu maswali mbalimbali ya wabunge kuhusu matumizi ya Kiswahili fasaha katika vyombo vya habari, Waziri na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wameliambia Bunge kuwa, ni vyema sasa hata wamiliki wa vyombo vya habari wakaanza kuzingatia ufaulu kwa somo la Kiswahili kabla ya kuwaajiri waandishi.
Kwa upande wake Waziri Nape akitoa majibu ya nyongeza, alisema kuenziwa kwa Kiswahili nchini kumeipa Tanzania hadhi ya kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za Afrika zinazojihusisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments