Tundu Lissu Kagoma Kula Hadi Polisi Wamfikishe Mahakamani
Wakati Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akigoma kula hadi afikishwe mahakamani, wakili wake amepeleka maombi Mahakama Kuu kuomba apewe dhamana baada ya polisi kuendelea kumshikilia kwa siku ya tatu.
Wakili wa mbunge huyo, Peter Kibatala alisema mteja wake amefikia hatua hiyo, baada ya Jeshi la Polisi linalomshikilia kumnyima dhamana bila sababu.
“Hakuna sababu za msingi za kumnyima dhamana na tangu jana Lissu hajala na amesema hatakula hadi afikishwe mahakamani,” alisema Kibatala na kuongeza:
“Kosa analodaiwa kulifanya lilifanyika Januari 4 na hadi Februari 6 ni mwezi, kama ni muda wa kuchunguza kosa hata hati ya mashtaka ingekuwa tayari,” alisema Kibatala.
Alisema mteja wao (Lissu) analalamikia kuanzia ukamatwaji wake ulipoanza, alipokamatwa eneo la Bunge bila Spika kuwa na taarifa.
Kibatala alisema polisi waliokwenda kumkamata aliwatambua njiani na alikamatwa bila kuwapo kibali cha kukamata (arrest warrant).
No comments