Waziri Mkuu: Rais Hajatangaza Kufutwa Kwa Vyama Vya Upinzani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Februari, 2, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake Mheshimiwa Mbowe alisema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vyama vya upinzani na ifikapo mwaka 2020 hakuna upinzani nchini.
Pia Mheshimiwa Mbowe alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Mbali na Mheshimiwa Lema, pia kiongozi huyo alitaka kujua kuhusiana na kufungwa kwa Mbunge wa Kilombelo, Mheshimiwa Peter Lijualikali pamoja na madiwani sita wa chama hicho ambao wamefungwa na viongozi wengine 215 wanakabiliwa na kesi mbalimbali.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani. Pia Watanzania wote wanajua nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu i,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “tunajua katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu ipo Serikali, Mahakama na Bunge na hakuna mhimili unaoweza kuuingilia mhimili mwingine,”.
“Pia Watanzania wote wanajua kwamba jambo lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali pengine popote, hivyo siwezi kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote yanayoendelea chini ya sheria na yaliyo mahakamani,” amesema.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea kuzalisha na hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.
“Hadi kufikia mwishoni mwa msimu wa uzalishaji ambao ni mwezi Machi, tunaweza kuwa tumefikia malengo na kama itajitokeza upungufu Serikali itatafuta namna nzuri ya kupata sukari kwa kushirikiana na wenye viwanda nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mheshimiwa Suleiman Sadiq aliyetaka kujua hali ya sukari ilivyo nchini kwa sasa na hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kunusuru hali ya uhaba wa sukari isijitokeze.
No comments