Ajali ya Moto London: Watu 12 wafariki, 18 wamo katika hali mahututi hospitali
Watu 12 wamethibitishwa kufariki na wengine 18 wamo katika hali mahututi hospitalini baada ya moto kuteketeza jumba la ghorofa 24 la makazi magharibi mwa London.
Moto huo ulizuka katika jumba hilo usiku wa kuamkia Jumatano. Jengo hilo bado linawaka moto na watu wengi hawajulikani walipo.
Taarifa za kwanza za kuzuka kwa moto jumba hilo la Grenfell Tower, kaskazini mwa Kensington ziliripotiwa saa, 00:54 BST (saa tisa kasoro dakika tisa Afrika Mashariki).
Watu 12 wamefariki kwa mujibu wa polisi, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Kuna watu 78 ambao wamepokea matibabu hospitalini. Hospitali sita – St Mary’s, Chelsea and Westminster, Royal Free, St Thomas’, Charing Cross Hospital na King’s College Hospital – zilipokea majeruhi.
Kamishna wa wazima moto wa London Dany Cotton anasema wazima moto kadha walipata majeraha madogo.
Walioshuhudia wanasema huenda kuna watu waliokwama kwenye jengo hilo, lililokuwa na nyumba 120 za makazi.
Diwani wa Notting Dale Judith Blakeman, anayeishi hapo karibu, anasema kumekuwa na watu kati ya 400 na 600 ambao wamekuwa wakiishi katika jumba hilo.
Meya wa London Sadiq Khan amesema wazimamoto walifanikiwa kufikia ghorofa ya 12 pekee.
Polisi wa jiji wametoa nambari ya dharura kwa watu wanaotafuta habari kuhusu jamaa na marafiki – 0800 0961 233.
No comments