Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alia na uchache wa wataalamu wa afya nchini
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kuwa ipo haja ya kuzalisha wataalamu zaidi ili kukwepa kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Amesema hayo jana Jumatatu, Julai 24, alipokuwa akizindua mkutano wa siku mbili uliozikutanisha nchi 12 zikiwamo za Afrika ili kujadili utoaji wa huduma za afya hususani katika sekta binafsi.
Alisema katika majukwaa ni rahisi kusema hakuna haja ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu, lakini kiuhalisia jambo hilo haliwezekani kwa sababu wataalamu waliopo ni wachache.
Alitolea mfano nchi nzima kuna wataalamu watatu wa upasuaji wenye utaalamu wa mishipa ya fahamu ambao hawatoshi ukilinganisha na idadi ya Watanzania wanaofikia 50 milioni.
Rais Kikwete pia alitumia mkutano huo kuwaasa wahudumu wa afya wa sekta binafsi kusisistiza matumizi ya bima ya afya kwa wananchi badala ya kung'ang'ania kudhaminiwa na Serikali kupata mikopo.
Alisema rais huyo mstaafu: "Msijisumbue kwa hili Serikali haiwezi kuwadhamini wala msijidanganye, haiwezi kufanya hivyo kwa sababu italazimika kutumia kodi za wananchi kulipa mikopo iliyowashinda kulipa.
“Wananchi wakiwa na bima ya afya mnaweza kujipanua hadi mikoani na mkafanya kazi na kuacha kufanya mijini pekee ambako wananchi angalau wanaweza kumudu gharama za matibabu," alisema.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa Mikopo-Afrika Mashariki Evelyne Gitonga alisema asilimia 84 ya vituo vya afya binafsi nchini Tanzania havifanyi vizuri kutokana na kukosa ruzuku kutoka serikalini na kutofikiwa na mikopo.
Alisema kukosekana mikopo na fedha za kujiendesha husababisha kutoa huduma chini ya kiwango hali inayosababisha wanaovitegemea kuendelea kuteseka.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema kuwa wataalamu wanazalishwa kwa wingi changamoto iliyopo ni ajira.
Alisema wanalifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha wanakuwa na rasilimali watu ya kutosha ili kufanikisha azma ya utoaji huduma bora ya afya.
No comments