Rais wa Shirikisho la soka Hispania na mtoto wake watiwa nguvuni na polisi
Takukuru ya Hispania inayojulikana kama Unidad Central Operativa, imewatia nguvuni rais wa Shirikisho la Soka Hispania (FA), Angel Maria Villar na mwanaye Gorka.
Ofisa wa taasisi hiyo, Judge Santiago Pedraz ndiye aliyesimamia zoezi zima wakati polisi walipokwenda kumkamata asubuhi ya leo.
Rais huyo wa Soka la Hispania, Maria Villar na mtoto wake wa kiume, Gorka wanashikiliwa kwa tuhuma kadhaa zikiwemo za matumizi mabaya ya ofisi, tuhuma za rushwa na nyingine zinazoelezwa kusababisha wizi wa fedha.
Ofisa wa taasisi hiyo ya kupambana na rushwa ya Hispania, Judge Santiago Pedraz ambaye alisimamia zoezi hilo, amesema wawili hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Pamoja na Villar na mwanaye, Makamu Rais wa masuala ya uchumi wa shirikisho hilo, Juan Padron, naye anashikiliwa.
Kama hiyo haitoshi, polisi wamefanya upekuzi katika ofisi za shirikisho hilo makao makuu na zile zilizo katika kisiwa cha Tenerife.
No comments