Urusi yadaiwa kudukua vitalu vya nyuklia vya Marekani
Wadukuzi wanaosadikika kuwa ni kutoka Urusi wamejaribu kudukua makumi ya vitalu vya nyuklia vya Marekani katika mwezi Mei na Juni, kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya usalama vya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Ulinzi ya Homeland ya Marekani (DHS), wadukuzi hao waliweka hatari kubwa kwenye vitalu hivyo vilivyopo Kansas.
Hata hivyo, vyombo vya ulinzi vya marekani na idara hiyo vilikataa kueleza kwa undani endapo vitalu hivyo vya nyuklia vilidukuliwa au udukuzi uliishia kwenye majaribio.
DHS wamesema wanalihusisha tukio hilo na wadukuzi wa Urusi kwani mbinu iliyotumika ni sawa na ile iliyotumika katika uchaguzi wa marekani pamoja na udukuzi wa vitalu vya nyuklia vilivyoleta madhara makubwa nchini Ukraine.
Idara hiyo ilieleza kuwa wadukuzi waliwatumia barua pepe maafisa wa ngazi za juu wa idara hiyo zilizosomeka ‘maombi ya kazi’, lakini zilikuwa zimebeba ‘codes’ ambazo zingewawezesha kufanya udukuzi huo baada ya maafisa hao kuzifungua.
Hata hivyo, msemaji wa DHS, Jenny Hageman alisema kuwa wadukuzi hao hawakuathiri utendaji wa vitalu hivyo.
“Ni kweli kwamba hawakuleta madhara kwa sababu mfumo wa kompyuta zinazotumika kwenye utendaji ni tofauti kabisa na mfumo mkuu,” Reuters imemkariri Hageman.
Marekani iliwahi kuituhumu Urusi kwa kufanya udukuaji kwenye vitalu mwaka 2015 vilivyopelekea kukatika kwa umeme katika nchi yote ya Ukraine.
Tuhuma za udukuzi dhidi ya Urusi zimetolewa saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kukutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Urusi, Vladimir Putin nchini Ujerumani walipokuwa wakihudhuria kikao cha G20.
No comments