Wanafunzi 3,637 waacha masomo kwa kupata ujauzito
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito.
Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akiahirisha mkutano wa Bunge mjini Dodoma.
“Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki, kuchimba madini,” alieleza Majaliwa.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito. Msimamo wa serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati.
“Msimamo huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Lengo hili lina nia ya kuwahimiza wazazi wawafundishe watoto wao mambo mema,” alifafanua.
Hata hivyo hivi karibuni, Rais Magufuli alipiga marufuku wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo na kuwataka wale wanashabikia hilo wanaanzisha shule zao.
No comments