Jarida la Economist: Mji wa Lagos wa pili mbaya zaidi kuishi duniani
Mji wa Lagos nchini Nigeria umeorodheshwa wa pili mbaya zaidi kuishi duniani na jarida la The Economist la mwaka 2017.
Jarida hilo, katika ripoti yake ya Global Liveability Report ya mwaka 2017, imeorodhesha mji mkuu wa Syria, Damascus ambao umeathiriwa sana na mapigano kuwa ndio mbaya kuishi ukiushinda mji huo mkuu wa kibiashara wa Nigeria.
Mji bora zaidi kuishi duniani ni Melbourne nchini Australia.
Lagos ni miongoni mwa miji mitano kutoka bara la Afrika ambayo imo miongoni mwa miji 10 hatari zaidi kuishi duniani.
Miji hiyo mingine ni mji mkuu wa Libya, Tripoli, mji mkuu wa Algeria, Algiers, mji mkuu wa Zimbabwe, Harare na mji mkubwa zaidi nchini Cameroon, Douala.
Orodha hiyo huangazia mambo matano: uthabiti, huduma ya afya, utamaduni na mazingira, elimu na miundo mbinu.
Kuna mji mmoja Afrika hata hivyo ambao umeimarika pakubwa.
Abidjan, mji mkubwa zaidi nchini Ivory Coast, uliorodheshwa kuwa miongoni mwa miji mitano iliyoimarika pakubwa tangu kuandaliwa kwa ripoti kama hiyo miaka mitano iliyopita.
No comments