Kikwete Awatetea Wapinzani......Ataka Wasichukuliwe kama Maadui
Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyama tawala barani Afrika kutovichukulia vyama vya upinzani kama maadui wa serikali badala yake vionekane kama moja ya nguzo muhimu katika kutimiza utawala wa sheria.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wabunge wa vyama tawala pamoja na viongozi wengine, kuvikosoa vyama vyao pale vinapokwenda mrama badala ya kuwa waoga na kuunga mkono mambo yote.
Rais Kikwete ambaye ni maarufu Tanzania kwa jina la JK ameyasema hayo alipokuwa katika mkutano wa masuala ya uongozi barani Afrika wa mwaka 2017 (African Leadership Forum 2017) ambao umefanyikia nchini Afrika Kusini.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Rais mstsaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na Rais mstaafu wa Malawi, Bakili Muluzi.
Akizungumza katika kongamano hilo la siku mbili lililomalizika Agosti 25, 2017, JK alisema kuwa, kuvichukulia vyama vya upinzani au wanasiasa wa upinzani kama maadui, ni kutengeneza uadui ambao hauna ulazima katika nchi za Afrika.
Kikwete alisema kuwa vyama vya upinzani katika nchi nyingi za Afrika vina kazi kubwa ya kuhakikisha vinanadi sera zao kwa wananchi ili viweze kufahamika zaidi kwa vingi ni vichanga. Hii itasaidia wananchi kuwa na uelewa wa sera pamoja na mipango yao inapofika wakati wa uchaguzi wakiomba dhamana ya kuongoza nchi, alisema JK.
Mbali na wito huo kwa watawala, Rais Kikwete alivitaka vyama vya upinzania pia kukubali matokeo ya uchaguzi endapo umefanyika katika mazingira ya haki, uhuru na uwazi.
Kazi ya vyama vya upinzani ni kuhakikisha kuwa serikali inakuwa macho muda wote kutekeleza majukumu yake, lakini na wao wasiwe watu wa kupinga au kukataa kila jambo.
Kauli hii ya Rais Kikwete imekuja wakati ambao vyama vya upinzani nchini vinalalamika kuhusu kuzuiwa kwa mikutanao ya kisiasa, maandamano, pamoja na kukamatwa mara kwa mara kwa viongozi wa vyama vya upinzani.
Kwa upande wake Rais Mzee Mkapa, alivitaka vyombo vya habari na waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa nchi zao wanapofanya kazi na waandike habari zitakazochochea maendeleo ya wananchi pamoja na kuzikosoa serikali kwa nia ya kujenga.
No comments