Usikose Hizi Hapa

RAIS MAGUFULI AMTEUA PROFESA LUOGA KUWA GAVANA MPYA WA BENKI KUU YA TANZANIA(BOT)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amemteua mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Makinikia, Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchukua nafasi ya Prof. Benno Ndulu aliyekuwa akiushikilia wadhifa huo.
Rais Dk. Magufuli ametangaza uteuzi huo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati ya Makinikia iliyofanikisha kufikiwa makubaliano ya kihistoria baina ya serikali na kampuni ya Barrick Gold yaliyofungua ukurasa mpya kwa Tanzania kunufaika zaidi na madini ya dhahabu.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wenyeviti wa kamati za bunge za madini ya Almasi na Tanzanite, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.

Rais Dk. Magufuli alimshukuru Spika wa Bunge na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha hati ya dharura sheria ya madini.

Kwa upande wake Gavana mteule Profesa Florens Luoga amesema atafanya kazi kwa uweledi kama sheria za nchi zinavyoelekeza na kuomba ushirikiano kwa wataalamu wengine wa mambo ya fedha ili kuinua uchumi wa taifa.

Aidha, Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwashangaa watu wanaozusha kuwa mapato ya nchi yamepungua na kusema kuwa huo ni uongo kwani haiwezekani serikali ikafanya miradi mikubwa ya ununuzi wa ndege kujenga reli ya kisasa, kujenga mradi wa umeme wa Stiegler Gorge kama mapato ya nchi yangekuwa yameshuka.

No comments