Usikose Hizi Hapa

SERIKALI KUPITIA WAZIRI MWIJAGE WAMJIBU DANGOTE

Serikali kupitia kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage imekanusha madai yaliyotolewa na Aliko Dangote kuwa, sera za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli zinatishia wawekezaji.
Akizungumza na gazeti la The Citizen jana, Waziri Mwijage amesema kuwa sera za uwekezaji ziko wazi na zina lenga kuhakikisha kuwa, serikali pia inanufaika na rasilimali za nchi.

Dangote ambaye ni tajiri namba moja Afrika alinukuliwa akisema kuwa, serikali imeweka sera ambazo zinaifanya imiliki asilimia kubwa ya hisa kwenye mali.

"Wanawatisha wawekezaji wengi, na kuwatisha wawekezaji sio kitu kizuri kufanya," alisema Dangote katika mkutano wa Afrika uliofanyika jijini London.

Dangote ni miongoni mwa wawekezaji Tanzania ambapo anamiliki kiwanda cha saruji chenye thamani ya Tsh 1.3 trilioni katika Mkoa wa Mtwara.

Waziri Mwijage alisema kuwa, wawekezaji katika Sekta ya Uchimbaji  wanatakiwa kutoa umiliki wa asiliimia 16 kwa serikali ili kuhakikisha kuwa nchi inafaidika kutokana na rasilimali zake. Aliongeza waziri huyo kwamba, anategemea mtu kama Dangote ambaye ni mwekezaji mkubwa nchini, awe na uelewa kuhusu sheria za nchi.

"Kampuni inapokuja kuwekeza katika sekta ya uchimbaji, hisa za serikali hazitakiwi kuwa chini ya asilimia 16, na hili si kosa kabisa kwa sababu rasilimali ni zetu," alisema Waziri Mwijage.

Aidha, Waziri Mwijage alisisitiza kuwa atahakikisha wawekezaji wote nchini wanafuata sheria, na kwamba hakutegemea kama Dangote angekuwa mmoja wa watu ambao wangekosoa mazingira ya uwekezaji Tanzania.

“Dangote amekuwa hana tatizo hapa. Wakati wowote anapokumbwa na tatizo, serikali yote hukimbia na kumsaidia. Unakumbuka alipokuwa na tatizo mwaka jana, wote tulikuwepo kwa ajili ya kumsaidia,” alisema Waziri Mwijage.

Katika mkutano huo, Dangote alisema uhusiano wake na Rais Magufuli ni mzuri, lakini akamshauri kuangalia upya sera zake za uwekezaji.

No comments