Usikose Hizi Hapa

ZITTO KABWE AIOMBA CHADEMA IMWACHIE UWANJA AJIPIME NA CCM

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi mdogo wa madiwani, Chama cha ACT Wazalendo kimeviomba vyama vingine vya upinzani kukiachia kipambane na CCM katika kata mbili kati ya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo uchaguzi utafanyika.
Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017 utahusisha kata 43 nchini, Dar es Salaam ukihusisha za Saranga, Kijichi na Mbweni.

ACT Wazalendo imesema utafiti iliyoufanya unaonyesha chama hicho kinaweza  kuchukua kata za Kijichi na Saranga endapo vyama vingine vya upinzani vitakiachia kisimamishe wagombea watakaochuana na wa CCM.

Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Oktoba 28,2017 jijini Dar es Salaam amesema ACT Wazalendo imeamua kuwasimamisha wagombea wawili na kuiachia kata moja kwa vyama vingine vya upinzani kwa kuwa wamejipima na kuona wanaweza kushinda bila kupingwa Kijichi na Saranga.

“Tumefanya utafiti mdogo kule Mbweni tukaona vyama vikuu vitatu ni ACT, Chadema na CCM tukaona upo uwezekano wa sisi na Chadema kugawana kura, tumeona tuwaachie kata ile,” amesema.

Zitto amesema, “Tumejipima na kuona ACT ikisimama peke yake Kijichi na Saranga tuna uwezo wa kuishinda CCM asubuhi kweupe. Tunachoomba vyama vingine vya upinzani vituachie tusimamishe wagombea halafu tushirikiane nao kuhakikisha tunaiangusha CCM.”

Amesema, “Tunawaambia wenzetu upinzani adui yetu ni mmoja CCM, hivyo tuweke kando tofauti zetu tushirikiane lengo ni kuhakikisha katika kata tatu za Dar es Salaam, CCM haipati hata moja.”

No comments