Usikose Hizi Hapa

MTOTO WA CHACHA WANGWE AHUKUMIWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mtoto wa Marehemu Chacha Wangwe ambae alikua Mbunge wa Tarime, Bob Chacha Wangwe kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela au kulipa faini ya Shilingi Milioni 5 baada ya kupatikana na hatia kwenye kosa la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Facebook.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo amesema katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 6 na vielelezo 5 dhidi ya Bob ambae pia ni Mwanaharakati.

Alisema kuwa Mei 7, 2016 polisi walipata taarifa ya chapisho la Bob ambapo walianza kumfatilia na kumkamata kisha walichukua simu na kuipeleka maabara ya Polisi ili kuikagua.

“Kimsingi Bob hukupinga kuandika maneno hayo lakini umedai kuwa hukuyachapisha katika jamii bali yalikuwa ni siri kwenye akaunti yako“.

Hakimu Shaidi alisema kuwa wakati wa ushahidi simu yake ilipokaguliwa ilionekana ilitumika kuchapisha ujumbe huo kwa jamii na watu walimjibu, ikiashiria ujumbe uliwafikia.

“Hivyo ni dhahiri ulikuwa na nia ya kuchapisha taarifa hiyo, kueleza kile ambacho ulikiona sahihi kama ingekuwa ni ujumbe wako binafsi basi Polisi wasingeweza kukutafuta na watu wasingekujibu“

Hakimu Shahidi amesema kutokana na hatua hiyo Bob amekutwa na hatia chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015 ambapo katika utetezi wake, Bob aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni Mwanafunzi wa masomo ya Sheria na pia ni kijana mdogo na ni kosa lake la kwanza kulitenda.

Hakimu Shaidi alisema anakubaliana na hoja za Bob kwani Mahakama inamuona bado ni mdogo na anapaswa kufanya mambo mengi mazuri katika jamii ambapo pia amesema kama yeye ni mwanafunzi wa masomo ya sheria anapaswa kufanya mambo mema katika jamii vitu ambavyo wengine watamuiga.

“Hivyo Mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh.milioni 5 ama uende jela mwaka mmoja na nusu na pia milango ya dhamana ipo wazi“

Katika kesi hiyo namba 167, Chacha Wange anatuhumiwa kwa kosa la kuchapisha taarifa za kupotosha katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook March 15,2016 ambapo aliandika maneno yafuatayo hapa chini.

“….Tanzania ni ambayo inajaza chuki wananchi.… matokeo ya kubaka Demokrasia Zanzibar ni hatari zaidi ya Muungano wenyewe…. Haiwezekani nchi ya Zanzibar kuwa koloni la Tanzania Bara kwasababu za kijinga.”

No comments