Usikose Hizi Hapa

WATU 6 WASHIKILIWA KWA KUKUTWA NA MIFUPA YA ALBINO, ULIMI WA SIMBA

Watu sita wanashikiliwa na polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za kukutwa na vipande vitatu vya mifupa ya mtu wanayedai kuwa ni albino, pamoja na mafuta na ulimi unaodhaniwa kuwa wa simba.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mathias Nyange alisema jana kuwa watu hao walikamatwa juzi saa 7:00 mchana katika mji wa Tunduma wilayani Momba na askari waliokuwa doria.

Alisema watuhumiwa hao walikutwa na mafuta ya simba, mifupa mitatu ya albino, mfupa mmoja wa mnyama ambaye hajajulikana, na vipande viwili vya ulimi, vitu vinavyosadikiwa kuwa ni vifaa vya tiba asili.

Kamanda Nyange alidai kuwa baada ya kuhojiwa, watuhumiwa walikiri kuwa mifupa waliyokutwa nayo ni ya albino waliyemkata mkono mkoani Morogoro.

Alisema kati ya watuhumiwa hao wawili ni wakazi wa Morogoro, wawili wakazi wa Mbozi, mmoja ni mkazi wa Wilaya ya Momba na mwingine ni kutoka Nakonde nchini Zambia.

Nyange alisema watuhumiwa hao wanatarajia kupelekwa mkoani Morogoro ambako ndiko wanakotuhumiwa kutenda kosa.

Wakati huohuo, Nyange amesema watu watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 30 wamefariki dunia baada ya kupigwa risasi na askari waliokuwa doria saa 4:00 usiku wa Novemba 30 baada ya kukaidi amri ya kusimama ya polisi ambao waliwatilia shaka.

Baada ya kukataa kutii amri ya kusimama, polisi waliwafuatilia na baadaye watu hao walianza kuwafyatulia risasi, jambo ambalo kamanda huyo alisema liliwalazimisha askari kuanza kujibizana nao.

Alisema baada ya kuwapekua walikutwa na silaha moja aina ya bastola iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za short gun ikiwa na risasi moja na pia walikutwa na mapanga mawili pamoja na kipande kimoja cha nondo.

No comments