ASKARI MAGEREZA ATIWA MBARONI KWA KUMPIGA RISASI YA KICHWA ASKARI MWENZAKE
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia askari wa Jeshi la Magereza, Faustine Masanja, kwa tuhuma za kumwua kwa kumpiga risasi askari mwenzake, wakiwa kazini.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea jana asubuhi katika eneo la Magereza, Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Ombeni Mwakiyani.
Alisema siku ya tukio wakiwa kazini, Faustine alidaiwa kumjeruhi askari mwenzake ambaye alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
“Tukio limetokea asubuhi…Faustine alimjeruhi mwenzake wakiwa kazini na baada ya kumjeruhi alipelekwa hospitalini kupata tiba ila alifariki dunia.
“Tunachunguza kubaini nini hasa chanzo cha kumjeruhi mwenzake na kumsababishia kifo,” alisema Kamanda.
Mmoja wa askari magereza aliyeshuhudia tukio hilo, alidai Masanja na Mwakiyani wameoa katika familia moja na inadaiwa kulikuwa na ugomvi wa familia kati yao.
Chanzo hicho kilidai asubuhi wakiwa kazini, Faustine alimpiga mwenzake risasi ya nyuma ya kichwa ambayo ilitokea usoni.
“Wameoa familia moja na wote wanakaa kambini na Faustine aligombana na mke wake ambaye ameondoka nyumbani hivyo akawa anamtuhumu marehemu kupitia mke wake kuwa walimjaza mkewe maneno na kusababisha aondoke nyumbani.
“Baada ya kumpiga mwenzake risasi alitupa silaha yake chini na kusema akamatwe wala hakimbii kwa sababu anajua ameua. Ila ugomvi wenyewe hatujajua ulikuwa ni nini hasa,” kilisema chanzo.
No comments