HIZI NDIZO SABABU ZILIZOMFANYA MWENYEKITI WA UVCCM KURUDISHWA RUMANDE
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis ambaye alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili yanayohusu rushwa, amekosa dhamana mpaka Jumanne ijayo kwa hofu ya kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu wa umoja huo .
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar alifikishwa mahakamani hapo majira ya 4:55 asubuhi na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Joseph Fovo, mwendesha mashtaka wa Takukuru, Biswaro Biswaro alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake maeneo ya kata ya Mnadani, Manispaa ya Dodoma.
Alisema katika kosa la kwanza, Sadifa akiwa nyumbani kwake alitoa rushwa ya vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa UVCCM, Rashid Mohamed Rashid.
Biswaro alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi ya kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma–Kagera kama zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.
Wakili huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shabani, Abdallah Hamimu, Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John Lufunga, Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel Shitobelo, Happiness Rynyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha Domisian na Hashim Abdallah.
Biswaro alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) na (2).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Fovo alimhoji mshtakiwa huyo ambaye alikana kutenda makosa yote mawili.
Biswaro alisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na upande wa Jamhuri unaweka pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa.
Mwendesha mashtaka Biswaro alisema sababu za kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo ni kutokana na mkutano mkuu wa uchaguzi UVCCM kuwa wa siku mbili mfululizo, juzi na jana na pia matokeo yakiwa bado hayajatangazwa.
Alisema endapo Sadifa atakuwa nje kuna uwezekano wa kuingilia uchaguzi huo.
“Naomba Mahakama itambue uchaguzi bado unaendelea na mshtakiwa hadi sasa hajakabidhi uongozi... bado ni mwenyekiti,” alisema Biswaro.
Aidha, Biswaro alisema sababu nyingine ni kuwa mashahidi wengi ni viongozi ambao ni wenyeviti na makatibu na endapo akiachiwa kwa dhamana ana kila aina ya ushawishi unaoweza kuvuruga upelelezi.
Kufuatia maelezo hayo, wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alipinga kuzuiwa kwa dhamana na kudai kuwa ni haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alibainisha kiapo cha kuzuia dhamana hicho kilichowasilishwa mahakamani ambacho kimetolewa na Kamanda wa Takukuru mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, hakina mashiko.
“Uchaguzi wa UVCCM umeshaisha na mshindi tayari ameshapatikana na hakuna uchaguzi mwingine wa kuingilia au kama kuna uchaguzi utafanyika, kiapo kingesema,” alisema Wasonga.
Alihoji sababu za kupelekwa mahakamani kwa kesi ambayo upelelezi wake haujakamilika na kuzuia dhamana kwa mshtakiwa.
Alisema mshtakiwa huyo hataweza kuingilia uchunguzi kwa sababu walizozitoa.“Hawa mashahidi atawezaje kuwashawishi wakati mtu ameshatoka madarakani?" Alihoji wakili Wasonga."Mteja wangu ni Mbunge, ni mtu makini na anaaminiwa. Asihukumiwe kwa kuwekwa ndani kwasababu zisizo na mashiko.”
Aliomba mahakama itupilie mbali pingamizi hilo na mshtakiwa apewe dhamana kwa kuwa hataweza kuingilia uchaguzi kwa kuwa uchaguzi mwingine wa UVCCM utafanyika mwaka 2022.
Kutokana na mvutano huo wa kisheria, Hakimu Fovo aliahirisha kesi hiyo hadi Jumanne ijayo ndipo mahakama itatoa maamuzi kuhusu suala hilo. Alisema mshtakiwa ataendelea kuwa rumande.
No comments