IDADI YAONGEZEKA WALIOKUFA MAJI ZIWA TANGANYIKA
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoa wa Kigoma, Amaniel Sekulu amesema miili sita ya watu waliozama katika ajali ya boti kugonga mtumbwi katika Ziwa Tanganyika imeopolewa.
Mpaka sasa idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea Ijumaa iliyopita imefikia 19 kutokana na awali kuopolewa miili 13.
Akizungumza leo Jumapili Desemba 24, Sekulu amesema miili hiyo sita imeharibika kutokana na kukaa majini zaidi ya saa 50.
Amesema uopoaji wa miili hiyo ilikumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo wazamiaji kukumbana na hali mbaya ya hewa, mvua za mara kwa mara, mawimbi makubwa na kina kirefu cha maji.
Amesema Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na wananchi wenye ujuzi wa kuogelea ndio waliofanikisha kupatikana kwa miili hiyo.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia Ijumaa ikihusisha boti la Atakalo mola lililokuwa linatoka Kigoma mjini kwenda Kalya na mtumbwi wa MV Pasaka uliookuwa ukitoka kijiji cha Kalilani kwenda Sunuka.
MV Pasaka ilikuwa imebeba waumini wa Kanisa la Pentekoste waliokuwa wanakwenda kwenye mkutano wa injili na sherehe za sikukuu Krisimasi katika kijiji cha Sunuka.
No comments