MATUKIO YA KIHALIFU YAMEPUNGUA MWAKA HUU - DCI ROBERT BOAZ
Jeshi la Polisi limesema matukio ya kihalifu kwa
mwaka huu,yamepungua kutoka 68,204 yaliyoripotiwa mwaka 2016 hadi kufikia
matukio 61,774 kwa mwaka 2017 huku likisema hali ya usalama imezidi kuimarika.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa makosa ya
jinai -DCI, Robert Boaz alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya
muenendo wa hali ya Usalama wa nchi hususani kuelekea mwishoni mwa mwaka.
Akizungumzia tukio la kupotea kwa mwandishi wa
Gazeti la Mwananchi,Azory Gwanda,Boaz amesema wanachukua kila hatua, na
kuwaomba wananchi wawe na subira wakati jeshi linaendelea kuchukua taratibu
zinazotakiwa.
Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani DCI- Boaz
amesema yamepungua kutokana na matukio yaliyoripotiwa ni 9,550 katika kipindi cha januari mpaka novemba mwaka 2016 ikilinganishwa na na matukio 5,537 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2017 ambapo kuna upungufu wa matukio 4,013 sawa na asilimia 42.
Ajali hizo zilisababisha vifo vya watu 3,108 na majeruhi 8,898 kwa mwaka 2016 wakati mwaka huu 2017 vifo vya watu ni 2,491 na majeruhi 5,696
Hata hivyo ameongeza kuwa pamoja na uhalifu kupungua mwaka huu,bado kuna changamoto za makosa dhidi ya binadamu ambayo yanajumuisha ubakaji,kulawiti, wizi wa watoto mauaji ,kunajisi pamoja na kusafirisha binadamu ambapo makosa hayo ya jinai yameongezeka kutoka 11,513 mwaka 2016 hadi kufikia 11,620 mwaka huu 2017 ambayo ni ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.
No comments