Usikose Hizi Hapa

TTCL YACHACHAFYA KUFUATIA SAKATA LA AIRTEL...YASIMULIA MASAA 24 YALIVYOTUMIKA KUWALIZA WATANZANIA

Ikiwa imepita siku moja tangu Rais John Magufuli amwagize Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuchunguza undani wa suala la umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel, siri zaidi kuhusiana na kile kilichofanyika katika ‘dili’ za mauziano zimeanza kuanikwa.

Akizungumza mjini Dodoma juzi, Rais Magufuli alimtaka Dk. Mpango kuchunguza  undani wa kampuni ya Airtel baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa kampuni hiyo inapaswa kuwa chini ya umiliki wa Kampuni ya Simu (TTCL),  ambayo ni ya serikali. Pia Rais Magufuli alieleza wazi kuwa kuna ‘mchezo mchafu’ uliofanywa na baadhi ya watu katika suala hilo.

Kutokana na agizo hilo la Rais Magufuli, jana, TTCL, kupitia kwa mwenyekiti wake wa sasa wa bodi ya wakurugenzi, Omar Nundu, na Ofisa Mtendaji Mkuu, Waziri Kindamba, iliibuka na kuanika undani wa mambo kadhaa kuhusiana na kampuni hiyo, mojawapo ikiwa namna vigogo watano walivyoketi kwa siku moja na kufanya uamuzi unaoibua maswali mengi kwa sasa kuhusiana na umiliki wa kampuni ya Airtel. Kimahesabu, siku moja ina saa 24.

Alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo linaloambatana na madai kwamba TTCL ndiyo inayoimiliki Airtel Tanzania, Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Jackoson Mbando, alisema jambo hilo hawawezi kulizungumzia kama watendaji bali wamiliki wa hisa walio nje ya nchi ndio wenye wajibu huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nundu alisema  chanzo cha yote kilianzia Agosti 5, 2005, wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi za TTCL na Celtel wakati huo na wajumbe watano ambao majina yao hakuwa tayari kuyataja, walipokutana siku hiyo moja na kubariki uamuzi mzito uliofikisha jambo hilo lilipo sasa.

Nundu alisema bodi hiyo ilikuwa na watu tisa, lakini siku hiyo moja waliketi watano kati yao na kufanya uamuzi huo mazito huku wakiongozwa na mwenyekiti ambaye wakati huo alikuwa amekabidhiwa asilimia moja ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na ‘mtu asiyejulikana’.

Nundu alisema Celnet ilianzishwa na TTCL Mei 7, 2001 kwa mtaji wa Sh. bilioni moja na thamani ya hisa ikiwa Sh. milioni moja.

Alibainisha kuwa TTCL ilikuwa ikimiliki hisa moja huku thamani ya hisa ilikuwa Sh. 1,000 na mtu asiyejulikana alikuwa akimiliki hisa moja yenye thamani pia ya Sh. 1,000, kuanza baishara kwa jina la Celtel.

Hata hivyo, Nundu alisema hisa moja ya mtu asiyejulikana ikashikiliwa na raia wa kigeni na kwamba baadaye, TTCL ilitoa bilioni tano kwa ajili ya mtaji ili kampuni ianze kufanya kazi.

"Ilianzishwa kampuni inaitwa Celnet…imeanzishwa na TTCL,…ikapewa masafa megawati 900. Ilipofika wakati wa kufanya kazi, ikabadilishwa na kuwa Celtel, kampuni hii ilianzishwa na TTCL Mei 7, 2007 mtaji wake ukiwa Sh. bilioni moja, maana yake hisa milioni moja na kila hisa ina thamani Sh. 1,000,” alisema Nundu.

“Lakini wanahisa wakawa wawili, TTCL yenyewe ikachukua hisa moja, mtu asiyejulikana akachukua hisa moja, lakini akaishika raia wa kigeni. Kwa maana hiyo, kampuni ikaanzishwa kwa fedha Sh. 2,000," alisema Nundu.

Aidha, Nundu alisema TTCL ilitoa pia fedha zaidi ya Sh. bilioni 82 kwa ajili ya biashara huku cha kushangaza, mtu asiyejulikana akiwa hajatoa kitu chochote.  

"Kama si TTCL kutoa Sh. bilioni tano,  hakuna ambacho kingefanyika. Hakukuwa  na uhitaji wa mwekezaji…. isitoshe TTCL iliweka Sh. bilioni 82 na ushee kuikopesha Celtel…sasa hapo unaona ni kampuni ya TTCL," alisema Nundu.

Alisema baadaye, raia wa kigeni aliyekuwa akishikilia hisa moja ya mtu asiyejulikana aliikabidhi kwa Mtanzania ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na pia Celtel. 

“Siku ya kikao hicho, mwenyekiti wa bodi (ambaye ndiye aliyekabidhiwa hisa hiyo moja ya mtu asiyejulikana) na wajumbe wengine watano walifanya maamuzi (uamuzi) magumu (mgumu) ya kuirudisha hisa hiyo moja na kuikabidhi TTCL, hivyo TTCL ikawa inamiliki Celtel kwa hisa zote kwa asilimia 100,” alisema.

Akieleza zaidi kuhusiana na ‘mchezo’ uliofanyika, Nundu alisema thamani ya hisa asilimia 100 za TTCL ilikuwa Sh. bilioni moja, lakini wakakubaliana siku hiyo kuongeza thamani ya hisa hizo hadi kufikia Sh. bilioni 50 katika kampuni ya Celtel.

Alisema mpaka Mei 7, 2001, hisa 999,998 zisizo na mtu ilipewa TTCL kwa sababu ilishaweka Sh. bilioni tano, hivyo kuwa na jumla ya hisa 999,999 huku mtu asiyejulikana akiwa bado anamiliki hisa moja.

Nundu alisema ilipofika Novemba 27, 2001, raia wa kigeni aliyeshikilia hisa ya mtu asiyejulikana alimpa mtu mwingine ashikilie ambaye ni Mtanzania, na mtu huyo aliyepewa ashikilie ndiye aliyekuwa mwenyeki wa bodi ya TTCL na Celtel.

Nundu aliongeza kuwa baada ya hapo, zilichukuliwa Sh. bilioni 40 za TTCL na kuwekwa katika mfuko wa Celtel kama mtaji wake, hivyo kuifanya kumilikiwa kwa asilimia 100 kwa mtaji wa Sh. bilioni 41, huku Sh. bilioni tisa zikiwa hazina mmiliki.

“Siku hiyo hiyo moja, baada ya muda TTCL ikanyang’anywa hisa zake zote  na hapo ndipo tunapojiuliza uhalali wa Celtel,” alisema Nundu.

Nundu alisema kama  hiyo haitoshi, hisa hizo zilianza kugawanywa kwa watu ambao hawapo katika mlolongo wa Celtel kutokana na ukweli kuwa wakati huo,  waliokuwa wakitambulika ni wawili tu, yaani TTCL na ‘mtu asiyejulikana’.

Aidha, alisema ilikubaliwa kuwa serikali ipewe asilimia 65 na ‘mtu asiyejulikana’ apewe asimilia 35.Alisema kwa hesabu za kawaida, haikupaswa watu wengine kugaiwa hisa kwa sababu hawakuwa na hisa tangu awali lakini wakapewa hisa zote.

Alisema kama haitoshi, siku hiyo hiyo ya kikao cha bodi yenye watu watano, serikali ikapewa hisa milioni 26.650, ikiwa ni uwiano wa asilimia 65 ya umiliki na mwingine (mtu asiyejulikana) alipewa hisa milioni 14.350, sawa na asilimia 35.

Baada ya hapo, alisema serikali ilichukua tena hisa milioni 10 zingine na kumpa mwekezaji, hivyo kumfanya afikishe milioni 24.350 na kuifanya serikali kubakiwa na hisa milioni 16.650.

Alisema uwiano huo ndio unaoendelea hadi leo na kwamba umiliki wa Celtel upo mikononi mwa Airtel ‘kimagumashi’ (kijanjaujanja).

Kadhalika, Nundu alisema jambo la kushangaza ni kwamba ilipofika Juni 23, mwaka jana, Airtel ilitangaza kujitoa kwenye umiliki wa TTCL ambao walikuwa wamiliki na wameshajitoa.

Nundu alisema baada ya kufanyika ‘mchezo’ huo,  TTCL ilikopeshwa dola za Marekani milioni 28 na kuwekewa riba ya asilimia 18 na kusababisha deni kukua hadi kufikia Sh. bilioni 76.6.

“Mimi na wenzangu baada ya kuja TTCL, ndiyo tukaanza kuchimba chimba ili kujua mbivu na mbichi kwa sababu kuna mambo mazito zaidi,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema wanachotaka kutoka kwa Airtel ni kampuni yao.

Alisema wanaamini na kutarajia kuwa watarejeshewa kampuni yao bila kukwaruzana na wamikili wa kampuni ya Airtel na kwamba wamejipanga kwa ushahidi wa asilimia 100.

“Tumeamua kujitoa sadaka za nafsi na miili yetu kwa ajili ya kutetea wanyonge katika vita hii kubwa ya uchumi inayoongozwa na Rais Magufuli,” alisema Kindamba.

Pia alisema wanatarajia kufanya biashara ya huduma za simu kwa gharama nafuu zaidi watakaporejeshewa kampuni yao na pia kuiwezesha kulipa kodi zaidi serikalini.

No comments