Kampeni zaingia dosari, mmoja achomwa mkuki Morogoro
Kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zimeanza kuingia dosari baada ya mfuasi wa Chadema, Martha Maenda (33) mkazi wa Kichangani, Manispaa ya Morogoro kuchomwa mkuki mkono wa kulia tukio linalohusishwa na masuala ya kisiasa.
Maenda aliyelazwa wodi namba tatu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, alichomwa mkuki juzi saa 10:00 alfajiri, tukio linalohusishwa na uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kiwanja cha Ndege mkoani hapa.
Akizungumza akiwa hospitali, Maenda alisema akiwa pamoja na wenzake wakiandaa chai kwenye kambi ya Chadema iliyopo Mtaa wa Kimunyu, walivamiwa na watu wenye silaha za jadi ambao anadai ni wafuasi wa CCM.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma alikana chama hicho kuhusika akitaka Chadema waseme ukweli wa kilichotokea.
“Nikiwa na wenzangu tukiandaa chai, lilipita gari dogo lililosimama usawa wa nyumba tuliyoweka kambi; waliteremka wanaume wasiopungua wanne waliokuwa na mapanga, rungu, sime, fimbo, mkuki na kutuvamia,” alidai Maenda.
Alidai wenzake walikimbia, yeye alipojaribu alikamatwa na mmoja wa vijana hao aliyemchoma mkuki mkono wa kulia akiwa chini baada ya kuanguka.
Baadaye watu hao walitoweka kwa kutumia gari. Mganga msaidizi wa wodi aliyolazwa Maenda, Dk John Muneja alithibitisha kumpokea majeruhi huyo saa 11:00 alfajiri.
Msemaji wa Chadema wilayani Morogoro, Shaaban Dimoso alisema tukio hilo linalenga kudhoofisha kampeni za chama hicho na kwamba, siyo la kwanza kwani Januari 13, saa mbili usiku kuna mtu alivamia kambi hiyo akiwa na panga lakini alidhibitiwa na taarifa ilitolewa polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce Ferdinand alithibitisha kupokea taarifa za mtu mmoja kujeruhiwa na mkuki na uchunguzi unaendelea.
Wakati hayo yakitokea Morogoro, wananchi wa Kata ya Ngarenanyuki wilayani Arumeru mkoani Arusha, wamepinga kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuweka mashada ya maua kwenye kaburi la Naftari Ndekirwa, aliyekuwa diwani wa kata hiyo aliyefariki kwa ajali ya kuangukiwa na mti.
Mkazi wa Kijiji cha Olkung’wado, Anael Naftari alisema kitendo cha kwenda kumsalimia mjane na kuweka mashada ya maua baada ya msiba kumalizika muda mrefu linamzidishia uchungu.
Mkazi mwingine, Ndekirwa Urasa alisema hayo yanafanyika yakiwa ni mtaji wa kisiasa ili kupata kura. Katika uchaguzi huo, Chadema kimemsimamisha Aminiel Mungure kuwania udiwani, huku mgombea wa CCM ni Zacharia Nko.
Katika maeneo mengine ya kampeni, Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola aliwataka wakazi wa Kata ya Igombavanu kumchagua diwani wa CCM ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kigola alitoa kauli hiyo juzi akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Rashid Mkuvasa ambaye yeye alijinadi kwamba anao uzoefu na kazi hiyo kwa kuwa amekuwa diwani kwa kipindi cha miaka 10.
No comments