Usikose Hizi Hapa

Mapinduzi Cup Fainali leo ni Simba au Azam FC?



Fainali za 11 za michuano ya Kombe la Mapinduzi Cup zinatarajiwa kupigwa leo kwenye dimba la Amaan Visiwani Zanzibar kwa kuzikutanisha timu za Simba na Azam zote za Dar es Salaam.

Mchezo huo unaotarajiwa kuanza Saa 2:15 usiku wa leo, utakuwa ni wa pili kuzikutanisha timu hizo katika fainali ya michuano hiyo.

Awali zilikutana katika fainali ya mwaka 2012 na Azam FC ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutwaa taji lake la kwanza kati ya mawili ya Kombe la Mapinduzi, linguine likija mwaka 2013 baada ya kuifunga Tusker katika fainali.

Simba ndiyo mabingwa mara nyingi wa taji hilo, mara tatu baada ya kulitwaa katika miaka ya 2008 ikiifunga Mtibwa Sugar katika fainali, 2011 ikiwafunga mahasimu, Yanga na 2015 wakiwafunga Mtibwa Sugar.

Kocha wa Simba Joseph Omog, amepania kulitwaa taji hilo, kwa lengo la kuondoa ukame wa makombe ambayo umeikumba klabu hiyo kwa misimu minne iliyopita pasipo kubeba ubingwa wowote

Azam mara zote ilizoingia fainali ilitwaa taji hilo, wakati Simba mwaka 2012 na 2014 ilicheza mechi ya mwisho na kufungwa na kukosa Kombe hilo.

Kuelekea mchezo wa leo, kila timu iko vizuri baada ya rekodi nzuri katika mechi zilizopita, Simba wakiwatoa wapinzani wa jadi, Yanga kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali na Azam wakiitoa Taifa Jang’ombe kwa bao 1-0.

Timu zote ziliongoza makundi yao, Simba A lilikuwa na timu tano kwa pointi zake 10 na Azam B lililokuwa na timu nne kwa pointi zake saba.

No comments