Sehemu ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere(JNIA) Yateketea kwa moto usiku wa kuamkia leo
Moto mkubwa umezuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA)
usiku wa leo na kusababisha taharuki kubwa kwa wasafiri na watumiaji wa uwanja huo, ambapo imelazimu shughuli zote uwanjani hapo kusitishwa kwa muda wakati vikosi vya zimamoto vikiendelea na kazi yao kwenye uwanja huo mkubwa zaidi nchini Tanzania.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Martin Otieno amesema kuwa wamefanikiwa kuudhibiti moto huo na kwamba uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha moto huo na hasara iliyosababisha, unaendelea kufanyika na kwamba tayari shughuli zote za kawaida zinaendelea kama kawaida.
Aidha Meneja wa Uwanja huo ameeleza kuwa kwa sasa shughuli zote za usafirishaji zimeamishiwa Terminal One na zinaendelea kama kawaida huku wakiweka sawa maeneo yalioathirika.
“Kwanza naomba niwatoe hofu Watanzania na wasafiri wote wanaotumia Uwanja wetu, ni kweli moto umezuka kuanzia majira ya saa 6 hadi saa 7 usiku wa kuamkia leo.
“Lakini madhara kidogo yametokea kwenye jengo la kuhifadhia mizigo pekee, hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa kutokana na moto, mashine zote zipo salama na sasa shughuli zote za usafirishaji tumezihamishia kule terminal one (Uwanja wa zamani) zinaendelea kama kawaida”. Amesema Meneja huyo.
“Baada ya kuudhibiti moto huo tumerudi kuangalia chanzo tukakuta, mfumo wa umeme uko sawa, hivyo hatujajua chanzo hasa cha moto huo ila tunajitahidi kufanya utafiti ili tujue.” Aliongeza Meneja na kusema taarifa zaidi, zitatolewa baadaye.
No comments