Muumini Apigwa risasi nje ya kanisa akisubiri ibada Ubungo
Muumini wa kanisa Katoliki, Adrian Mpande amepigwa risasi mbili akiwa anasubiri kuingia kanisani katika Parokia ya Kibangu wilaya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa George Ng’atigwa ambaye ni shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa Mpande alikuwa akisubiri kuingia kanisani majira ya saa tatu asubuhi lakini alikuja mtu mmoja aliyekuwa anatembea kwa miguu na kumpiga risasi ubavuni na mkononi, hali iliyosababisha aanguke na kupoteza fahamu.
Alisema kuwa mtu huyo alikimbia lakini watu waliokuwa maeneo hayo walifanikiwa kumkamata baada ya kuishiwa risasi wakati akijaribu kuwatishia.
Aliongeza kuwa baada ya kumkamata mtu huyo, waliwasiliana na jeshi la polisi ambalo lilifika na kuondoka naye kwa ajili ya taratibu za kisheria na kwamba majeruhi alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupatiwa huduma ya kwanza katika zahanati iliyokuwa karibu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Dar es Salaam, Suzan Kaganda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa limetokana na ugomvi wa kifamilia.
“Mtuhumiwa tunaye tunaendelea kumhoji na aliyejeruhiwa yuko hospitali anaendelea na matibatu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,”Kamanda Kaganda anakaririwa.
No comments