Mwana FA na AY Waendelea Kutamba Mahakamani
Wasanii wakongwe wa Bongo Flava, Ambwene ‘AY’ Yesaya na Hamisi ‘Mwana FA’ Mwinjuma wameendelea kupeta mahakamani wakitarajiwa kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 2.1 na kampuni ya Mic Tanzania Limited.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Kampuni hiyo ya huduma za simu za mkononi iliyotaka kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga amri ya kutakiwa kuwalipa wasanii hao kiasi hicho cha fedha.
Hivi karibuni, Mahakama Kuu ilihalalisha uamuzi wa Mahakama ya Wilaya iliyoikuta na hatia ya kutumia bila kibali nyimbo za wasanii hao kama miito ya simu na kuitaka kuwalipa kiasi hicho cha fedha.
Wakili wa wasanii hao, Albert Msando aliweka pingamizi akiiomba Mahakama Kuu kuyakataa maombi yaliyowasilishwa na wanasheria wa kampuni ya Mic kwa madai kuwa ni batili kwani yalikuwa na makosa ya kisheria.
Jaji Isaya Arufani wa Mahakama Kuu alikubaliana na maelezo ya Wakili Msando na kuyatupilia mbali maombi ya wanasheria wa kampuni hiyo. Bado haijafahamika kama watafanya marekebisho na kurejesha maombi mapya au la.
AY na Mwana FA wanadai kuwa kampuni ya Mic Tanzania Limited ilitumia bila ruhusa yao nyimbo zao ‘Usije Mjini’ na ‘Dakika Moja’.
No comments