Rais Magufuli Atishia Kuifunga Migodi ya Madini Endapo Barrick Watachelewa Katika Mazungumzo
Wakati Kampuni ya Acacia ikisema imepoteza mapato ya Sh385 bilioni katika kipindi cha miezi sita kutokana na kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini nje, Rais John Magufuli ametishia kufunga migodi ya wawekezaji iwapo hawatajitokeza mapema katika mazungumzo.
Rais Magufuli amesema hayo takriban wiki moja baada ya kudokeza kuwa Serikali ingeanza mazungumzo “na waliokuwa wanatuibia” mapema wiki hii.
Jana, Rais Magufuli alisema Serikali haitasita kufunga migodi yote ya madini ambayo wamiliki walitakiwa kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu ulipaji kodi.
Akizungumza katika ziara yake mkoani Kigoma ambako alizindua Barabara ya Kibondo-Nyakanazi, Rais Magufuli alisema Taifa linapoteza fedha nyingi kutokana na upotevu wa madini.
“Ni matrilioni ya fedha ambayo yanapotea, na sasa hivi tumewaita tufanye mazungumzo lakini wakichelewachelewa nitafunga migodi yote,” alisema.
Alisema ni bora migodi hiyo ikakabidhiwa kwa Watanzania kuliko wawekezaji ambao hawalipi kodi.
Rais Magafuli alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga huo nje ya nchi, na baadaye kuunda kamati mbili; moja ya kuchunguza kiwango cha madini kilichokuwa katika makontena 277 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam na nyingine kuangalia athari za kiuchumi na kisheria tangu mchanga huo uanze kusafirishwa mwaka 1998.
Ripoti ya kamati ya kwanza ilisema kuwa Acacia, inayoendesha migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, haikusema ukweli kuhusu kiwango cha dhahabu, ikidai kuwa imebaini mchanga huo una madini hayo mara kumi ya kiwango kilichotangazwa na wawekezaji hao.
Ripoti ya kamati ya pili ilionyesha kuwa katika kipindi cha miaka 20, Serikali ilipoteza zaidi ya Sh108 trilioni na kwamba Acacia haijasajiliwa nchini na hivyo inafanya kazi kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Acacia haijakubaliana na matokeo ya ripoti hizo, ikisema inataka uchunguzi wa kamati huru na kwamba kama matokeo hayo ni ya kweli, Tanzania ingekuwa moja ya nchi tatu zinazozalisha dhahabu kwa wingi duniani.
Jana, Acacia ilisema imepoteza Sh385 bilioni katika kipindi cha miezi sita. Acacia pia imesema endapo hali itaendelea kuwa hivyo, italazimika kuufunga mgodi wake wa Bulyanhulu na kusitisha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi.
Hata hivyo, katika taarifa yake ya jana inayozungumzia kipindi cha Januari mpaka Juni, Acacia imesema imepata changamoto kubwa katika utendaji wake nchini.
“Nusu (ya kwanza), imetupa changamoto kubwa katika shughuli zetu Tanzania baada ya kuwekewa zuio la usafirishaji wa makinikia kuanzia Machi,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia, Brad Gordon. “Mapato yetu yameshuka mpaka dola 175 milioni za Kimarekani kutoka dola 318 milioni tulizotarajia.”
Licha ya kushindwa kuingiza Dola 175 milioni za Marekani (zaidi ya Sh385 bilioni) zilizotarajiwa, Acacia inasema imelipa dola51 milioni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambazo ni zaidi ya Sh112.2 bilioni.
Ili kulinda masilahi ya wanahisa wake, Acacia imewasilisha notisi kwa msuluhishi kwa ajili ya migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi ambayo ndiyo inayozalisha mchanga wa madini kwa sasa.
Buzwagi imekuwa ikisafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuuyeyusha ili kupata mabaki ya dhahabu, shaba na fedha kutokana na teknolojia hiyo kutokuwapo mgodini.
Hatua ya kwanza ya kuchenjua dhahabu hufanyika mgodini na mchanga unaosalia ndio unaosafirishwa nje. Acacia imekuwa ikieleza kuwa mchanga huo una asilimia 0.02 ya dhahabu wakati shaba ni asilimia 10.
Acacia pia imekanusha taarifa ya kuwapo amri ya kutakiwa kuondoka nchini kwa mmoja wa wafanyakazi wake wa kigeni.
“Hatuna taarifa za kutolewa kwa amri hiyo kwa mfanyakazi wetu yeyote wa kigeni aliyepo Tanzania. Tunashirikiana vizuri na Serikali kwenye mazungumzo yanayoendelea na hakuna aliyekamatwa habari hiyo si sahihi,” inasema taarifa hiyo.
No comments