Usikose Hizi Hapa

AZAM FC YALAZIMISHWA SARE NA SIMBA CHAMAZI

AZAM FC imeshindwa kutumia vyema fursa ya kucheza nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Simba SC katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba SC inayofikisha pointi nne sawa na Azam, inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, baada ya Prisons nayo kulazimishwa sare ya 2-2 na Maji Maji ya Songea leo Uwanja wa Sokoine, Mbeya.


Simba ndiyo waliouanza mchezo huo kwa kasi na kiu ya kusaka bao la mapema na katika dakika ya nne tu, mshambuliaji Nicholas Gyan alikaribia kufunga kama si mpira aliopiga kwa kichwa baada ya pasi ya kiungo Muzamil Yassin kuokolewa na kipa wa Azam, Mghana mwenzake, Razack Abalora.

Nahodha wa Azam FC, Himid Mao Mkami alionywa kwa kadi ya njano dakika ya 10 na mwamuzi Ludovick Charles kwa kumchezea rafu kiungo Mghana, James Kotei.


Kipa wa Simba SC, Aishi Manula aliokoa mashuti mawili mfululizo ya nyota wa Azam kutoka Ghana, kwanza Enock Atta Agyei dakika ya 18 na baadaye Yahya Mohammed dakika ya 32.


Simba wakajibu mashambulizi hayo dakika ya 37 kupitia kwa kiungo wake kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye naye shuti lake liliokolewa na kipa Mghana wa Azam, Razack Abalora.


Kipindi cha pili, Azam FC wakakianza kwa kasi na kiu ya kusaka mabao na dakika ya 55 Yahya Mohammed akapiga nje akiwa kwenye nafasi nzuri kabla ya Simba kujibu dakika ya 56, baada ya mshambuliaji wake, John Raphael Bocco kubinuka vizuri tik-tak akijarbu kumalizia krosi ya kiungo wa Muzamil Yassin, lakini kipa wa Azam, Abalora akaokoa.


Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akapiga nje dakika ya 64 kabla ya kiungo wa Simba, Said Ndemla aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Shiza Kichuya aliyeumia kupiga juu ya lango dakika ya 70.


Refa Ludovic Charles akamuonyesha kadi ya njano beki Mzimbabwe wa Azam anayeweza kucheza kama kiungo pia Bruce Kangwa dakika ya 72 kwa ubishi. Refa huyo wa Mwanza akawaonyesha kadi za njano pia viungo Mcameroon wa Azam, Stephan Kingue dakika ya 78 na Mghana James Kotei wa Simba kwa kuchezeana rafu.


Sure Boy tena dakika ya 87 akaikosesha Azam bao baada ya kupiga nje kufuatia pasi nzuri ya Yahya Mohammed. Dakika ya 89, beki Salim Mbonde akaonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Yahya Mohammed.


Kwa ujumla timu timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa kucheza kwa kukamiana kunaweza kuwa kulichangia matokeo ya sare, kwani muda mwingi zilitumika nguvu kuliko maarifa.  


Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Daniel Amoah/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk63, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Yahya Mohammed, Mbaraka Yussuf/Yahya Zaid dk72 na Enock Atta Agyei/Frank Domayo dk46.


Simba SC; Aishi Manula, Ally Shomary, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Method Mwanjali, James Kotei, Haruna Niyonzima, Muzamil Yassin, John Bocco, Nicholas Gyan/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk80 na Shiza Kichuya/Said Ndemla dk67.

No comments