Usikose Hizi Hapa

MAHAKAMA KUU YAMTAKA JOSEPHINE MUSHUMBUSI KATIKA KESI YA LULU MICHAEL

Kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii wa fani ya uigizaji filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu imeahirishwa hadi kesho Jumatano Oktoba 25,2017.
Kuahirishwa kwa kesi hiyo leo Jumanne Oktoba 24,2017 kunatokana na Jaji Sam Rumanyika kuamuru polisi aliyechukua maelezo ya shahidi Josephine Mushumbusi kufika mahakamani.

Awali, Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lulu katika kesi hiyo aliieleza Mahakama Kuu kuwa shahidi huyo hapatikani kwa kuwa yuko nchini Canada.

Kibatala aliiomba Mahakama iyapokee maelezo yake kama sehemu ya ushahidi.

Wakili wa Serikali, Faraja George alisema hapingi kuwasilishwa maelezo hayo mahakamani, bali anapinga kuwasilishwa na wakili Kibatala kwa kuwa yeye si aliyeyaandika.
 
Shahidi huyo ni wa pili wa upande wa utetezi baada ya Lulu kujitetea jana Jumatatu Oktoba 23,2017. Alijitetea  baada ya Jaji Rumanyika kusema ana kesi ya kujibu.

Lulu ambaye yupo nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi ya kumuua bila ya kukusudia msanii wa filamu, Steven Kanumba.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.

No comments