Rais Magufuli: Makonda Kwangu Ni Msomi Mzuri
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amesisitiza kuwa hakuja kuuza sura bali kufanya kazi na kwamba mke wake akimpenda inatosha kwake.
Rais Magufuli amesema hayo jana alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na kudai kuwa mkutano huo ni muhimu sana kwake kwakuwa Serikali za Mitaa ziko karibu zaidi na wananchi.
Alisema watu wengi waliokuwa wananufaika na rasilimali za nchi hawawezi kumpenda hata kidogo kwa mambo anayoyafanya lakini mke wake anatosha kabisa kumpenda kwani hakuja kuuza sura.
Akitolea mfano wa rasilimali za nchi, Rais Magufuli alisema hakuna nchi ambayo mnaweza kuona rasilimali zenu zinachukuliwa halafu mnaacha na kushangilia.
Alisema ndio maana kwenye Tanzanite wameamua kujenga uzio utakaogharimu sio zaidi ya shilingi bilioni sita (6).
Ndani ya siku chache tu baada ya ujenzi wa ukuta kuanza, uzalishaji wa Tanzanite umeongezeka takriban mara 30 zaidi na kwamba kuna siku itapatikana zaidi ya kilo 18 za Tanzanite, kiwango ambacho hakijawahi kutokea hapo awali.
Alisema katika mikataba ya madini, unakuta kabisa imeandikwa ‘hawa watu wasilipe ushuru’ na ni Mtanzania ametia saini.
“Mimi ndiye Rais na ninajua siri zote za nchi hii, ni kuguswa tu na Roho Mtakatifu hadi kushindwa kuwataja, na nikizungumza hivi waliokuwa wananufaika hawawezi kunipenda,” alisema.
Aidha, amemsifu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa mambo makubwa anayofanya ikiwemo vita dhidi ya madawa ya kulevya.
“RC Dar alipojaaribu kupambana na vita ya madawa ya kulevya ikawa kubwa kwake, na wanasema hajasoma, mimi hata kama hajui A lakini anakamata madawa ya kulevya, kwangu ni msomi mzuri,”amesema.
Rais Magufuli alimuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwaambia wakuu wengine wa mikoa kuiga mfano wa Makonda ambaye anasikia ameweza kukusanya Milioni 186.
“Nasikia Mhe. Makonda umekusanya Milioni 186 na ninamuona anavyohangaika, Waziri Mkuu kwanini viongozi wengine hawawezi kuiga kwa mwenzao?” amehoji Rais Magufuli.
Aliwapongeza ALAT kwa kuamua kuhamia Dodoma ambapo Waziri Mkuu ameshahamia na Makamu wa Rais amebakiza miezi 2 tu kuhamia, na yeye pia atahamia huko mwakani na kuonya kuwa sasa aje amuone mtu atakayebakia Dar es Salaam.
No comments