SIMBA NA STAND UTD ZAPIGWA FAINI KATIKA MECHI YAO
Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imezitwanga faini ya Sh 500,000 kila moja klabu za Simba na Stand United.
Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na wachezaji wake kuvaa jezi zenye namba tofauti na zile zilizosajiliwa. Wachezaji hao walivaa namba tofauti kwenye mechi namba 40 dhidi ya Simba iliyofanyika Oktoba Mosi, mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Stand United ilikiuka Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu inayelekeza kuwa kila mchezaji atatumia namba ya kudumu ya jezi iliyosajiliwa na klabu yake wakati wa maombi ya usajili. Adhabu dhidi ya Stand United ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.
Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kitendo hicho cha Simba ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu, na adhabu dhidi yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia Kamishna wa mechi hiyo, Maliki Tibabimale amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo hicho cha Simba.
Singida United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Adhabu dhidi ya Singida United imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu, wakati kitendo cha mashabiki wao ni kosa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu.
Nayo Stand United imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Simba, zote zilichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Katika mechi namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu, mashabiki hao waliwafanyia vurugu wachezaji wa Mbeya City wakati wakielekea vyumbani baada ya mchezo kumalizika, kabla ya Polisi kuingilia kati na kuwatawanua.
Adhabu hiyo ambayo ni sh. 500,000 (laki tano) kwa kila mechi imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Kamati imeionya klabu ya Stand United endapo vitendo hivyo vitatokea tena haitasita kuichukulia hatua kali zaidi za kikanuni
No comments