Usikose Hizi Hapa

MALKIA WA TEMBO : “KAULI YA JPM YA ‘HAPA KAZI TU’ HAITEKELEZWI MAHAKAMANI”

Raia wa China anayedaiwa kuwa malkia wa pembe za ndovu, Yang Feng Glan ameilalamika Mahakama kuhusu mashahidi wa upande wa mashtaka kutofika mahakamani licha ya kesi kupangwa kusikilizwa mfululizo.
Katika kuwasilisha malalamiko yake, amekariri kauli za Jaji Mkuu na Rais John Magufuli.

Yang ametoa malalamiko hayo leo Jumanne Novemba 7,2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akizungumza lugha ya Kiswahili, amedai alisikia Jaji Mkuu akisema kesi za muda mrefu lazima zimalizwe mwaka huu. Yang amesema kesi yake huwa inapangwa kusikilizwa mfululizo lakini hilo halijawahi kufanyika hata mara moja.

"Rais John Magufuli anasema hapa kazi tu, nikasema sasa Mahakama ile kazi haipo kwa haraka, nipo mahabusu naumwa moyo najitahidi nakuja," amesema Yang.

Ameomba kesi ikipangwa mashahidi wafike mahakamani akihoji iwapo shahidi mmoja anaumwa, na wengine wote wanaumwa?.

Yang ameeleza hayo baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kudai kuwa shahidi waliyemtarajia kutoka ushahidi bado anaumwa. Ameomba shauri hilo lipangiwe tarehe nyingine na wanaamini siku hiyo atakuwa vizuri.

Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko ameiomba Mahakama waendelee na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka ili kuokoa muda.

Wakili Wankyo alidai katika hali ya kawaida ni lazima shahidi huyo amalizie kutoa ushahidi wake kwanza ndipo wengine waendelee.

Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka kupeleka mashahidi wengine kama huyo hatakuwa ametengemaa kiafya.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Novemba 21, 24, 27 hadi 30 na Desemba Mosi, 2017.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase ambao kwa pamoja, wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014  walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889 zenye thamani ya Sh13 bilioni bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori.

No comments