WATAKWIMU NCHINI KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA UKUSANYAJI WA TAKWIMU BORA
Watakwimu nchini wametakiwa kuimarisha mbinu za uzalishaji wa takwimu kwa kutumia
teknolojia za kisasa ili kusaidia katika ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu
bora zitakazosaidia kupanga mipango ya maendeleo.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchumi kutoka Benki Kuu ya
Tanzania, Johnson Nyala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika na
kuwataka wadau waliopo kwenye mfumo wa utoaji na utumiaji wa
takwimu kushirikiana ili kupunguza kukosekana kwa ulinganifu wa takwimu.
“Matumizi ya
teknolojia yataipunguzia Serikali gharama za uzalishaji wa takwimu na kuongeza
ubora kutokana na mahitaji makubwa ya takwimu kwa matumizi mbalimbali,” alisema
Bw. Nyala.
Nyila
aliongeza kuwa takwimu bora za uchumi ni muhimu katika kupanga mipango ya
maendeleo na utungaji wa sera kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi.
“Wakati nchi
mbali mbali duniani ikiwemo Tanzania zimeanza kutekeleza agenda ya maendeleo
endelevu ya mwaka 2030, mahitaji ya takwimu bora za uchumi yanahitajika sana,”
alisema Bw. Nyila.
Kwa upande
wake Mkurugezni Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema
kuwa madhumuni makubwa ya kuadhimisha siku hii ni kuongeza uelewa wa umma juu
ya umuhimu wa takwimu katika nyanja zote za kimaisha ya kijamii na
kiuchumi.
Ameongeza kuwa
nchi mbalimbali za Afrika zilikubaliana kuadhimisha maadhimisho hayo kutokana
na uhitaji mkubwa wa ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu za uchumi
katika kuelekea utekelezaji wa Agenda ya Afrika ya mwaka 2063 na malengo ya
maendeleo endelevu ya mwaka 2030.
Siku ya
Takwimu Duniani huadhimishwa tarehe 20 Oktoba katika kipindi cha kila miaka
mitano ambapo kwa mwaka huu maadhimisho haya yameongozwa na Kauli mbiu
isemayo “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora”.
No comments