Usikose Hizi Hapa

TBA YAKIRI KUBOMOKA KWA MABWENI MAPYA YA UDSM YALIYOZINDULIWA NA JPM

Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo nchini Mhandisi Elius A. Mwakalinga, amekiri picha zinazosambaa mitandaoni zikionyesha majengo mapya ya mabweni ya UDSM yana nyufa ni za majengo hayo, huku akisema ni kitu cha kawaida kwa majengo makubwa.

Mwakalinga amesema kutokea kwa nyufa hizo ni moja ya hatua za 'expansion joint' ambazo hutumiwa kwenye ujenzi wa majengo, lakini majengo hayo yamekidhi vigezo vyote na vipimo wakati wa ujenzi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 4,2017 Mwakalinga amesema kwa kawaida udongo unaobeba jengo hutitia baada ya muda fulani, hivyo wakati wa ujenzi huacha nafasi kuliwezesha jengo kupumua bila kusababisha nyufa.

Mwakalinga amesema kuna makosa yalifanyika ya kuziba nafasi zilizoachwa (expansion joint) kwa kutumia saruji badala ya mbao au plastiki maalumu hivyo kuonyesha nyufa kwenye jengo hilo.

Amesema nyufa zimetokea sehemu mwafaka ambazo walitarajia na kwamba kila jengo lina expansion joint tatu kwa ajili ya usalama wa jengo.

Mwakalinga amesema majengo hayo ya hosteli za wanafunzi bado yako chini ya uangalizi wa TBA, kwa hiyo wataanza ukarabati na hakuna haja ya kuhamisha wanafunzi kwa sababu jengo liko imara.



"Kila design tunayofanya ya majengo sasa hivi tunatumia expansion joint, majengo mengi makubwa huwa inatumia hiyo, hivyo ni common na sio creck kubwa sana kama inavoonekana kwenye picha, nilienda ile jana usiku kukagua tukakuta hiyo hali, ni process za majengo ili yaweze kusatle, hivyo watu wawe na amani kabisa wala wasiwe na hofu", amesema Bwana Mwakalinga.

Amesema kwa taaluma ya ujenzi wa majengo, dosari hiyo ni ya kawaida kutokea na kwamba, wakala umeanza kuchukua hatua kuzisahihisha kwa kuhakikisha uwazi uliopo unakuwa huru bila kujazwa kitu kigumu.

Mwakalinga amesema ujenzi umegharimu Sh10 bilioni walizopewa na Serikali na kwamba fedha hizo zilitosha kwa sababu walizingatia hadidu za rejea walizopewa na Rais John Magufuli kwa ajili ya ujenzi.

Amesema wamejenga vyumba 960 vyenye uwezo wa kubeba wanafunzi 3,840 na kwamba, gharama ya vyumba hivyo ni sawa na Sh10.4 milioni kwa kila kimoja.

Mwakalinga amesema Sh10.8 bilioni zimetumika kujenga shule ya Ihungo mkoani Kagera iliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi ambayo itakuwa na nyumba 30 za walimu.

"Walijitokeza watu kujenga kwa Sh60 bilioni lakini sisi tumejenga kwa Sh10 bilioni tu. Kwa hiyo, inawezekana na sisi ndiyo tuliojenga, msiwasikilize wengine ambao hawana ujuzi wowote katika ujenzi," amesema.

Akizungumzia muda wa ujenzi, amesema hosteli hizo zilijengwa kwa miezi minane ambayo kitaalamu inatosha kwa ujenzi imara.

Amesema msingi wa mabweni hayo una uwezo wa kubeba ghorofa nyingine mbili zaidi na utaalamu ulizingatiwa katika ujenzi.

No comments