POLISI, TCRA WAZUNGUMZIA AKAUNTI YA MANGE KIMAMBI
Jeshi la Polisi limetaka liachwe liendelee kufanya kazi yake kwa weledi katika kushughulikia suala la Mtanzania aishiye ughaibuni, Mange Kimambi, ambaye anatuhumiwa kuchapisha taarifa zinazodaiwa kuwatusi mitandaoni watu mbalimbali wakiwamo viongozi.
Akizungumza na Nipashe kuhusiana na uwezekano wa wao kuifunga akaunti ya Kimambi ikiwa sehemu ya hatua wanazochukua kwa sasa, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alisema ni kweli jeshi lao linalifanyia kazi suala hilo.
Hata hivyo Mwakalukwa hakutaka kukubali au kukataa juu ya kile kilichodaiwa kutokea kwenye akaunti ya Kikambi na badala yake kutaka apewe muda wa kulifanyia kazi ndipo alitolee maelezo ya kina.
“Hili jambo lina mambo mengi sana. Watu wengi wanahusika na taasisi nyingi (pia) zitahusika kulishughulikia, Hivyo tunaendelea kupokea mawazo ya watu mbalimbali kuhusu namna ya kwenda nalo… mawazo wanayotupa tunayafanyia kazi lakini naomba mtuache kwanza tunaendelea kulishughulikia,” alisema Mwakalukwa.
Aidha wakati Msemaji wa Polisi akisema hayo, TCRA ilisema kuwa haiwezi kufunga wala kuingilia akaunti ya Kimambi kwa sababu huo siyo wajibu wake kisheria.
Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala, aliiambia Nipashe kuwa mamlaka yao haina nguvu za kisheria kufanya kazi hiyo bali wenye wajibu wa kufanya hivyo ni kitengo cha kudhibiti uhalifu wa mitandaoni cha Jeshi la Polisi.
Akifafanua zaidi, msemaji huyo alisema makosa yote yanayohusu mitandao, yakiwamo ya watu kutishiwa maisha, kutukanwa, kuibiwa kwa njia ya mtandao au kunyanyaswa kwa namna yoyote mtandaoni, wanaohusika ni polisi na siyo TCRA.
“Masuala ya akaunti za watu kwenye mitandao kama hiyo unayosema (ya Kimambi)… mwenye mamlaka ya kuingia na kuzifunga ni Jeshi la Polisi. Bunge liliipa mamlaka ya kisheria polisi kuchunguza na kukamata wahalifu kama hao… waulizeni wao,” alisema Mwakyanjala.
Hata hivyo zipo taarifa mitandaoni zilimkariri Mtanzania huyo aishiye Marekani kuwa kilichotokea ni matokeo ya kazi ya wadukuzi wa mitandaoni, maarufu kama ‘hackers’ kupoteza akaunti yake yenye wafuasi takribani milioni 1.5.
Pamoja na hayo upo ujumbe wa lugha ya kigeni uliokuwa ukisambaa kwenye mtandao wa instagram ukionyesha kuwa akaunti inayofahamika kuwa ni ya Kimambi, imefungwa na waendeshaji wa mtandao wa Instagram kwa sababu ya kuwapo kwa malalamiko dhidi ya machapisho ya akaunti hiyo.
No comments