Usikose Hizi Hapa

WAZIRI KIGWANGALA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BANDARINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam ambapo alibaini uwepo wa makontena yenye magogo ambayo ni mazao ya misitu yaliyokaa bandarini hapo kwa zaidi ya miaka 10.

Waziri Kigwangalla ameagiza Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii atangaze kujitokeza kwa wamiliki wa magogo hayo 938  na kama wamiliki wasipojitokeza, magogo hayo yatakuwa mali ya Serikali.

Aidha Dkt. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 yanayodaiwa kuingizwa nchini kutoka nchini Zambia kujitokeza na kuwasilisha nyaraka zao zenye kuthibitisha kama kweli yalivunwa nchini Zambia na yalivunwa wapi na kwa vibali gani vya nchi hiyo pamoja na kufuatilia nyaraka za kuingiza ndani ya Tanzania.
Ameagiza kitengo cha kuzuia ujangili kifuatilie kubaini uhalisia na uhalali wa taarifa hizo vinginevyo yatakuwa mali ya Serikali.

Dkt. Kigwangalla amefanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo kufuatia uwepo wa taarifa za uvunaji holela wa magogo nchini, ambapo kuna taarifa kuwa kuna wafanyabiashara wa kigeni wanagawa vifaa vya kuvunia bure kwa ahadi ya kuuziwa mzigo na wahusika, pia uwepo wa taarifa kwamba kuna baadhi ya watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanaotoa vibali na kugonga nembo kinyume cha taratibu za kisheria, hali inayotishia usalama wa raslimali adimu ya misitu yetu ya asili.

No comments