Usikose Hizi Hapa

UKAWA WALIVYOISHINDA CCM KIAJABU UNAIBU MEYA JIJINI DAR ES SALAAM

Diwani wa Kilawani, Mussa Kafana (CUF), ameibuka mshindi wa nafasi ya Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, huku matokeo hayo yuakiwashangaza wengi kwa kuwa idadi ya madiwani wa CCM walikuwa sawa na wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mshangao huo unatokana na hali ilivyotokea kinyume cha matarajio kwani kutokana na idadi ya madiwani wa CCM na upinzani, wengi walidhani kuwa huenda kura baina ya pande husika zingekuwa sawa. Katika uchaguzi huo, madiwani wa CCM walikuwa 11 kama walivyo wa Ukawa.

Pamoja na matokeo hayo, Kafana alipata kura 12 na kumshinda mpinzani wake, Mariam Lulida (CCM) aliyepata kura 10.

Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na mvutano wa muda mrefu kati ya Ukawa na CCM, katika kikao cha Baraza la Jiji, mgombea huyo wa CUF ililazimika kufikishwa ukumbini kushiriki kupiga kura licha ya kwamba ni mgonjwa.

Mvutano ulianza kutokea baada ya Kafana kushindwa kufika kwa madai alikuwa mgonjwa, hatua ambayo iliwafanya madiwani wa upinzani kugoma kujiorodhesha mpaka mgombea wao afikishwe ukumbini kwa kuwa hawana taarifa za kuumwa kwake.
Madiwani wa CCM kwa upande wao walikuwa wanagoma diwani Kafana kuletwa ukumbini kwa vile ni mgonjwa huku wapinzani wakidai kuna kuwa kuna mchezo ambao unafanywa na CCM ili usifanyike uchaguzi kwa vile taarifa za kuumwa hawazifahamu.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliingilia kati na kusisitiza kwamba mgombea huyo ni mgonjwa.

Licha ya kutoa taarifa hiyo, hali haikuwa shwari na ndipo madiwani wa upinzani walipotaka mgombea wao aletwe ukumbini hata kama ni mgonjwa na hatimaye kufikishwa akiwa amebebwa kutokana na hali yake.

Baada ya kufikishwa ukumbini alilazwa kwenye kiti hali ambayo iliwashtua baadhi ya wajumbe wakajikuta wanamwonea huruma.

Meya aliomba mwongozo wa kuahirishwa kwa kikao hicho kwa madai kuwa haikuwa halali kwa mgonjwa kufikishwa ukumbini kwa kuwa hali yake si nzuri.

“Baada ya kuona hali yake, naomba kikao hiki kiahirishwe, tukifanye siku nyingine. Limefanyika kosa kubwa sana kumleta mtu huyu hapa na menejimenti ifanye utaratibu wa kumpeleka hospitalini sasa hivi,” alisema.

Meya aliahirisha mkutano huo na mgonjwa kuamriwa kupelekwa hospitali, lakini baada ya mgonjwa kutolewa nje ya ukumbi, Mkurugenzi wa Jiji alisimama na kutaka kikao kiendelee na uchaguzi ufanyike kwa madai kwamba idadi imetimia.

Kutokana na kauli hiyo, madiwani wa Ukawa iliwalazimu kumbeba mgonjwa wao na kumrudisha ukumbini na alisaidiwa kupiga kura na Mbunge wa Ubungo, Saeed Kubenea, baada ya kikao hicho kuafiki.

Akimtangaza mshindi huyo, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, alisema wapigakura walikuwa 22, kura zilizopigwa zilikuwa 22 na hakuna kura iliyoharibika.

Alisema baada ya uchaguzi huo, Kafana alipata kura 12 na Lulida kura 10 ikiwa ni tofauti ya kura mbili, hivyo kumtangaza Kafana kuwa mshindi wa kiti hicho.

Baada ya matokeo kutangazwa , mshindi huyo ambaye alikuwa hajiwezi kutembea, alinyanyuka na kisha kutembea na kuingia katika gari lake.

No comments