Serikali Yaendelea Kujipanga Vizuri.......Watumishi Wote wa Umma sasa Kupokea Mishahara Kwa Wakati Mmoja
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angellah Kairuki, amesema katika mwaka huu mpya wa fedha watumishi wa umma watakuwa wanalipwa mishahara kwa wakati mmoja ili kupunguza matatizo ya mishahara yanayojitokeza.
Kairuki ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 18 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya mpya ya Ubungo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake aliyoianza jana katika halmashauri hiyo.
Amesema awali watumishi hao walikuwa wanapata mishahara yao kwa nyakati tofauti lakini sasa wataingizia mishahara yao moja kwa moja katika akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) badala ya kupitia benki za biashara.
"Hatutaki itokee huyu amewekewa mshahara tarehe 27, huku mwingine akienda kuangalia salio katika akaunti anaambiwa bado lakini sasa hivi itakuwa wakati mmoja," amesema Kairuki huku akishangaliwa na watumishi wa halmashauri hiyo.
Alisisitiza lengo la kuweka mfumo huo ni kuhakikisha watumishi wote wanapata mshahara wao wakati mmoja na hiyo itasaidia Serikali kusimamia kwa umakini mishahara.
Amefafanua kwamba siku tatu kabla mshahara haujaingizwa katika akaunti ya mtumishi, mwajiri sekta husika atapelekewa orodha ya watumishi watakaotakiwa kulipwa mishahara.
"Matumaini yangu waajiri watakuwa makini kuangalia orodha hizo ili isitokee hata mtumishi mmoja akaachwa," anasema Kairuki.
No comments