MAKALA: Vita ya Diamond na Alikiba ilivyoua nyimbo kali za Bongo Fleva zilizotoka mwezi septemba
Kuna msemo unasema fahari wawili wapiganao ziumiazo nyasi, huu msemo naufananisha na upinzani wa kimuziki uliopo baina ya wasanii wakubwa wa muziki wa Bongo Fleva, nchini Tanzania, Alikiba na Diamond Platnumz.
Upinzani ambao kwa upande mwingine umekuwa na faida kubwa kwa wasanii hao kwani wamekuwa wakipata shows, Matangazo na kuuza nyimbo kwa wingi mitandaoni hayo yote ni matunda ya uhasimu uliopo kati yao.
Lakini upinzani huo kwa kiasi fulani umekuwa ukiwaathiri wasanii wengine wakubwa na wachanga ambao nao wanapambana kila siku kuweza kupenya kwenye soko muziki.
Nakumbuka kipindi nikiwa Dodoma nilipata bahati ya kuongea na Mbunge wa Mtama, Mhe Nape Nnauye na kwenye mahojiano yake alizungumzia bifu iliyopo kati ya Diamond na Alikiba akiifananisha na upinzani wa timu kongwe za mpira wa miguu hapa nchini Simba na Yanga.
Kwa sababu gani Mhe. Nape aliwafananisha Diamond na Alikiba kama Simba na Yanga?Jibu ni kwamba timu hizo ndio zenye mashabiki wengi nchini ambapo zaidi ya asilimia 98% ya Watanzania ni mashabiki wa timu hizo huku timu nyingine zikibangaiza mashabiki.
Kilichomsukuma Nape Kufananisha hivyo ukweli ni kwamba uwepo wa upinzani wa kimuziki kati ya Diamond na Alikiba umepelekea baadhi ya Wasanii kukosa kabisa kuwa na mashabiki damdam (Loyal Fans) na kujikuta mashabiki wengi wakijigawa katika pande mbili za uteam Diamond na Alikiba.
Sio mbaya sana kwenye muziki wetu lakini tukubali kuwa kuna wasanii wa kizazi kijacho ambao ni wakali na kwa sasa walitakiwa wapate sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki ili kuonesha vipaji vyao ila wanakosa kuonekana.
Pia wapo wasanii wengine wakubwa na wametoa ngoma kali ila wameshindwa kusikilizwa na mashabiki hii yote ni kwa sababu kuna nyimbo mpya za Diamond na Alikiba zimetoka na mashabiki ndio wale wale wa Simba na Yanga ambao hawana muda kutazama mechi ya Ndanda FC vs Majimaji FC.
Hapa chini nimeorodhesha nyimbo 6 kali za wasanii wakubwa, ambazo zimetoka ndani ya mwezi septemba, lakini hazijapata mapokezi mazuri baada ya Alikiba kuachia wimbo wake wa Seduce Me na Diamond Platnumz kuachia wimbo wa ‘Zilipendwa’ akiwa na kundi zima la WCB na wimbo wake mpya wa Hallelujah aliowashirikisha Morgane Heritage aliouachia mwishoni wa mwezi septemba.
1-Me and You- Jay Moe.(wiki mbili views 67,653+)
Rapa mkongwe Jay Moe kwa kawaida video zake huwa hazitazamwi na watu wengi kivile kwani hata video zake za ziliomrudisha kwenye chart za ‘pesa madafu’ na ‘Nisaidie kushare’ zina zaidi ya miezi 6 mtandaoni lakini hazijafikisha watazamaji milioni 1. Lakini ukiangalia kwa wastani nyimbo hizo zilivyotoka zilitazamwa na watu wengi ndani ya wiki mbili ukilinganisha na wimbo huu wa ‘Me and You’ ambao umetazamwa mara 67,796+ mpaka sasa.
2-MAKUzi By Nay wa Mitego.(Wiki mbili views 162,112+)
Huu nao ni wimbo ambao kwa ukubwa wake ulistahili kufanya vizuri sio tu kwa sababu ya ukakasi wa jina la ngoma bali ni kutokana na jina la Nay wa Mitego na promo aliyopiga kabla ya ngoma kutoka. Lakini hadi sasa tangia utoke septemba 12 una views 154,666+ mapokezi ambayo hayajaenda sawa na ukubwa wa wimbo huo.
3-Kiutani Utani- Young Dee.(Wiki mbili views 202,124+)
Wimbo wa Seduce me na zilipendwa hazijauacha salama wimbo huu wa Kiutani utani ingawaje wimbo huu umetoka katika kipindi ambacho Young Dee alikuwa bado yupo kwenye skendo za kuvuja kwa picha za utupu alizopiga na Amber Lulu.
4-Kihasara by Nikki wa Pili Ft Chin Bees.(Wiki moja na siku 5 ina views 100,433+)
Nikki wa Pili huwa hakosei kwenye ngoma zake nyingi anazofanya na hata huu wimbo ukiusikiliza ni wimbo ambao unashawishi watu kutokata tamaa na hata video yake imekuwa ya kiutafauti sana, kwani video imekuwa na uhalisia na uchanganyaji wa rangi wa kipekee hongera kwa Director Lucca Swahili. Video hiyo mpaka sasa ina views 96,283+ na imetoka tarehe 20 septemba mwezi ambao vita ya ‘seduce me’ na zilipendwa ilikuwa inaendelea mitandaoni.
5-Barnaba- Mapenzi Jeneza.(Wiki moja na siku mbili views 181,921+)
Moja kati ya nyimbo ambazo kali kuanzia ujumbe, melody na video pia zilizotoka mwezi huu huwezi kuacha kuutaja wimbo wa Mapenzi Jeneza ambao video yake imetoka Septemba 19 na mpaka sasa una views 181,921.
6–Cheche By Ommy Dimpoz.(Wiki moja views 384,311+)
Hakuna ubishi kuwa wimbo wa Cheche ni wimbo mkubwa sana kuanzia Audio na video ila mapokezi yake kwa upande wa video yamekuwa sivyo ndivyo, hii inaweza kuwa kuchelewa kutoka kwa video hiyo au kutokana na uteam uliopo kati ya Diamond Platnumz na yeye pamoja na rafiki yake wa karibu Alikiba.
Tukubali kuwa Ommy Dimpoz hapa katikati alivyoposti picha akiwa na mama yake Diamond Platnumz akiambatanisha na Caption yenye maneno mazito kitendo hicho kiliwakera watu wengi sana sio tu kwa mashabiki wa Diamond bali hata kwa baadhi ya mashabiki wake, wengi wakichukulia kama kitendo cha udhalilishaji hii inaweza kuwa ni ndio sababu kubwa video ya cheche mpaka sasa kusua sua mtandao.
Video hiyo ya Ommy Dimpoz ilikaa siku mbili tu kileleni kama video inayotrend namba moja lakini siku ya tatu baada ya Diamond Platnumz kuachia video ya wimbo wake mpya wa ‘Hallelujah’ iliporomoka hadi nafasi ya 10. nadiriki kusema kuingilia kwake vita ya maneno ya Diamond na Alikiba kumeiathiri kwa kiasi video yake ya cheche ambayo licha ya ukubwa wake wote kwenye game video hiyo imetazamwa na watazamaji 384,311+ kwa siku 8.
Hizo ndio baadhi ya video za nyimbo kali zilizotoka mwezi huu lakini hazijapokelewa vizuri baada ya Alikiba na Diamond kuachia ngoma zilizoleta mijadala na ushindani mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia mwishoni mwa mwezi agosti na mwezi wote wa septemba.
Ushauri kwa wasanii wa Bongo Fleva ili matatizo hayo yasitokee ni vyema mkawa kitu kimoja kwanza mkatoa tofauti zenu kisha mkapeana muda wa kuachia ngoma, hii itasaidia sana kwanza kazi zenu kupokelewa vizuri na mashabiki pili kupeana sapoti kwa urahisi. leo hii sina uhakika kama Nikki wa Pili atatoa sapoti ya kupromoti wimbo wa Jay Moe ‘Me and You’ au wa Ommy Dimpoz ‘Cheche’ ile hali wimbo wake mpya unachechemea, ni muda wa kuungana kwa pamoja ili tuupeleke muziki wetu mbele.
Kumbuka orodha hii ni ya video za nyimbo ambazo hazijapokelewa vizuri kwenye mtandao wa Youtube na sio kwenye Redio au TV.
COPYRIGHTED BY BONGO 5
No comments