Usikose Hizi Hapa

POLISI YAENDELEA KUKUNA KICHWA SAKATA LA NABII TITO

Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limesema bado linashauriana na vyombo vingine juu ya hatua za kumchukulia mkazi wa Mtaa wa Ng'ong'ona katika Manispaa ya Dodoma, Onesmo Machibya anayejiita 'Nabii Tito', ambaye anatuhumiwa kueneza chuki ya kidini dhidi ya watu wengine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto jana alisema bado jeshi hilo linamshikilia Machibya (44) kwa kuwa imethibitika ana ugonjwa wa akili.

Alisema polisi inashirikiana na vyombo vingine ili kujua hatua stahiki za kumchukulia.

Aidha, Muroto alisema jeshi hilo bado linawatafuta wake zake wawili pamoja na kijakazi wake wanaodaiwa kushirikiana naye kueneza alichosema chuki hiyo.

Muroto, alisema kwa kufanya hivyo, nabii huyo ametenda kosa kwa kukiuka kifungu cha sheria namba 129 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2002.

Alidai pia nabii huyo anaendesha shughuli zake kinyume cha Sheria ya Jumuiya, sura ya 337 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.

"Mtuhumiwa huyu amekamatwa baada ya kurekodi vipande vifupi vya matangazo ya video na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini nyingine na kuleta chuki dhidi ya watu wengine na kurusha kwenye mitandao ya kijamii; na pia kusambaza vipeperushi kwenye maeneo ya starehe," alisema Kamanda Muroto.

Pia alidai kuwa nabii huyo anatangaza imani ya dini inayokiuka maadili ya nchi na kufanya hadharani vitendo visivyofaa akitumia kitabu kitakatifu cha Biblia ambacho pia hafungamani nacho.

"Pia anatoa tafakari za Biblia zenye upotoshaji, kufanya vitendo vya udhalilishaji hadharani na kuchochea maovu katika jamii, anashirikiana na wanawake wawili anaodai kuwa ni wake zake, mmoja wao akiwa ni kijakazi," alisema Muroto.

Muroto alisema nabii huyo alikamatwa akiwa na majoho meupe yenye misalaba miwili yenye rangi nyeusi mbele na nyuma, vipeperushi 80, Biblia moja na msalaba pamoja na vifaa anavyotumia kutangaza imani yake.

Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Juni 23, 2014 alilazwa katika Hospitali ya Muhimbili na kutibiwa magonjwa ya akili.

"Aliruhusiswa kutoka wodini na daktari wake Dk. William na kutakiwa kurejea tena kwa uangalizi wa tiba Julai 9, 2014 lakini hakurejea na pia mtuhumiwa alifikishwa Hospitali ya Mirembe Dodoma kwa uchunguzi uliofanywa na Dk. Dickson Philipo na kugundulika kuwa ni mgonjwa wa akili wa muda mrefu," alisema Muroto.

Alifafanua hali ya kuwa mgonjwa wa akili lakini ameendelea kuhamasisha maovu yaliyo kinyume na maadili ya dini zote na desturi za Watanzania huku akionekana ni mtu mwenye akili timamu na kupata watu wanaomshabikia na kuambatana naye.

Miongoni mwa mahubiri ya Nabii Tito ni pamoja na kudai kuwa Biblia imeruhusu watu kunywa pombe na waume za watu kuoa wafanyakazi wao wa ndani.

No comments